1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Janga

Umoja wa Ulaya, Ujerumani kuisaidia Ugiriki

Lilian Mtono
9 Septemba 2020

Umoja wa Ulaya wapeleka maafisa wa ngazi za juu nchini Ugiriki na kuahidi msaada kwa wakimbizi baada ya tukio la moto kwenye kambi ya wahamiaji ya Moria.

https://p.dw.com/p/3iEZQ
Griechenland Großbrand im Flüchtlingslager Moria
Picha: Imago Images/Xinhua/P. Balaskas

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen alisema Jumanne usiku kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba amehuzunishwa sana na tukio hilo la moto kwenye kambi ya waomba hifadhi na kuongeza kuwa amemtuma mmoja wa makamu wake, Margaritis Schinas.

Soma pia: Kambi ya wahamiaji Ugiriki yateketea kwa moto

Aliandika, mataifa wanachama wako tayari kusaidia na kipaumbele chao ni usalama wa wale walioachwa bila ya makazi. Maelfu ya waomba hifadhi wameachwa bila makaazi kufuatia moto huo kwenye kambi iliyofurika pomoni ya Moria iliyopo kwenye kisiwa cha Lesbos, nchini Ugiriki.

Mapema Jumatano kulifanyika mkutano usio wa kawaida wa serikali katika kasri la Maximos ambalo ni makazi rasmi ya waziri mkuu wa Ugiriki na baada ya kumalizika kwa mkutano huo msemaji wa serikali Stelios Petsas alisema baadhi ya wawakilishi wa serikali wangezuru kisiwa hicho.

Griechenland Großbrand im Flüchtlingslager Moria
Mwanamke akiwa amesimam karibu n makaazi yalioharibiwa na moto katika kambi ya Moria.Picha: Reuters/A. Konstantinidis

"Waziri wa mambo ya ndani wa Ugiriki Takis Theodorikakos, waziri wa masuala ya uhamiaji na hifadhi Notis Mitarachis na rais wa taasisi ya kitaifa ya afya ya umma, NPHO Panagotis Arkoumaneas watakwenda Lesbos na baada ya tathmini ya hali ilivyo kwenye eneo hilo, watafanya mkutano na waandishi wa habari saa sita mchana huko Mytilene."

Ujerumani kuchukua baadhi ya wakimbizi
 

Ujerumani tayari imesema itaisaidia Ugiriki baada ya tukio hilo lililosababisha takriban watu 12,600 kukosa makazi. Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani Steve Alter ameandika kupitia twitter kwamba hatua hiyo inafuatia majadiliano ya kina na serikali ya Ugiriki tangu jana.

Baadhi ya majimbo ya Ujerumani kama Berlin tayari yamesema yatawachukua wahamiaji hao, lakini msemaji huyo hakueleza wazi iwapo waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer ataruhusu hilo.

Soma pia: Wakimbizi wajazana kuvuka mpaka kati ya Uigiriki na Uturuki

Awali waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani ambayo ni rais wa sasa wa Umoja wa Ulaya Heiko Maas alisema wako tayari na kutaka kuangazia mara moja namna watakavyoisaidia Ugiriki.

Maas ameandika kupitia ukurasa wa twitter kwamba hatua hizo zitajumuisha mataifa yaliyo tayari kugawana wakimbizi miongoni mwa walioathirika. Operesheni kubwa ya uokozi ilikuwa inaendelea hii leo katika kambi hiyo.

Wito umetolewa kwa mataifa wanachama wa Ulaya kuingilia kati kusaidia kuwatafutia makazi wakimbizi. Brussels imetangaza kuwasaidia watoto 400 na vijana miongoni mwa wakazi 12,000.

Mzozo wa Moria unaelezea mahitaji ya mageuzi katika sera ya uhamiaji ya Ulaya, mchakato uliozorota kwa muda mrefu kutokana na mgawanyiko baina ya serikali za mataifa wanachama.

Chanzo: Mashirika

Griechenland Großbrand im Flüchtlingslager Moria
Wakimbizi na wahamiaji wakibeba vitu vyao wakati wanakimbia moto uliozuka katika kambi ya Moria, kisiwani Lesbos, Ugiriki, septemba 9, 2020.Picha: Reuters/E. Marcou