1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waandaa operesheni kupambana na maharamia wa Kisomali.

Nyanza, Halima15 Oktoba 2008

Kutokana na kuongezeka kwa vitisho vya maharamia katika pwani ya Somalia, Umoja wa Ulaya umepanga kuzindua operesheni maalum mwishoni mwa mwaka huu, ili kuweza kupambana na maharamia hao.

https://p.dw.com/p/FZXB
Picha hii inawaonesha wananchi wa Somalia, ambao baadhi yao wanashutumiwa kwa vitendo vya kiharamia katika pwani ya nchi hiyo.Picha: picture-alliance/dpa

Umoja wa Ulaya umepanga kuzindua operesheni hiyo mwezi Desemba kwa kutumia vikosi vya jeshi la anga na majini, kwa ajili ya kupambana na maharamia hao wanaotishia amani katika pwani ya Somalia.

Katika kipindi cha mwaka huu tu, maharamia hao wameteka nyara meli zipatazo 30, kwa lengo la kutaka kulipwa fedha, hali ambayo imefanya njia hiyo ya maji kuwa ya hatari.

Maharamia hao pia katika kipindi hicho, wamepata kiasi cha fedha kilichokadiriwa kufikiwa dola milioni 18 hadi 30 kama malipo ya fidia ya kukombolewa wale waliotekwa.


Katika taarifa yake, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya Javier Solana amesema, ujumbe wa Umoja wa Ulaya jana, uliamua kwamba kamanda wa kikosi cha majini cha jeshi la Uingereza, Admeri msaidizi Philip Jones kuongoza operesheni hiyo na kwamba makao makuu ya operesheni hiyo yatakuwa London, Uingereza.

Operesheni hiyo pia itasaidia kutoa mchango muhimu kwa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP, kwa kuweza kulinda meli zinazobeba chakula ambazo zinakuwa katika hatari ya kuvamiwa na maharamia hao, pindi zinapopita katika eneo hilo la pwani ya Somalia.


Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, huhitaji msaada wa kijeshi kwa ajili ya kusindikiza meli zinazopeleka msaada wa chakula kuweza kusaidia watu takriban milioni 2.4 nchini Somalia.


Somalia mpaka sasa bado imekuwa ikikabiliwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe hali iliyosababisha maelfu ya watu kupoteza maisha, kupata ulemavu na wengine kadhaa kuyakimbia makazi yao.


Awali akizungumza baada ya mkutano wa Mawaziri wa Ulinzi wa Umoja wa Ulaya uliofanyika nchini Ufaransa, Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Herve Morin alisema nchi zipatazo 10 za Umoja wa Ulaya zimeonesha nia ya kutaka kushiriki katika operesheni hiyo ya kupambana na maharamia na kwamba mpango huo unatarajia kukamilika mwezi ujao.


Nchi hizo ni pamoja na Ufaransa yenyewe, Ujerumani, Hispania, Sweden, Ubelgiji, Uholanzi, Cyprus Lithuania na Uingereza.


Naye Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Franz Josef Jung, amefahamisha kuwa mataifa ya Umoja wa UIaya yamepanga kutoa manowari tatu, meli tatu za uchunguzi pamoja na meli ya mizigo.


Aidha amesema Ujerumani ina mpango wa kutuma manowari katika operesheni hiyo.


Katika siku za hivi karibuni maharamia hao wa Kisomali walifanikiwa kuteka nyara meli moja ya Ukraine inayojulikana kama MV Faina ambayo ilikuwa imebeba zana za kivita, ikiwemo vifaru 33, shehena hizo za silaha zimezua mtafaruku kwa nchi husika.


Maharamia hao bado wanashikilia meli hiyo wakitaka kulipwa fidia ya mamilioni ya dola na kutishia kuilipua iwapo hawatapewa fedha hizo.


Hata hivyo siku ya mwisho iliyowekwa na maharamia hao ilikuwa ni jana asubuhi, ambayo imepita bila ya kutokea kwa tukio lolote.


Aidha majeshi ya ulinzi katika jimbo linalojitawala la Puntland wamefanikiwa kuwaokoa wafanyakazi wa meli ya mizigo iliyokuwa imebeba saruji kutoka Oman kupeleka katika bandari ya Somalia ya Bosasso.


Wanajeshi hao, walifanikiwa kuwaokoa watu hao baada ya maharamia 10 walioiteka nyara kuzidiwa nguvu na kukimbia.