1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wahimiza Makubaliano ya Ubia wa Uchumi

P.Martin29 Julai 2008

Umoja wa Ulaya unazingatia kujiepusha kutafsiri Makubaliano ya mpito ya Ubia wa Kiuchumi-EPAsi kihofia baadhi ya nchi za Afrika Karibea na Pasifiki-ACP huenda zikabadilisha mawazo na kutotia saini makubaliano ya mwisho.

https://p.dw.com/p/EljE

Kwa mujibu wa waraka wa Kamisheni ya Ulaya,kazi ya kutafsiri makubaliano ya mpito ya EPAs katika lugha 23 zinazotumiwa rasmi katika Umoja wa Ulaya pamoja na kuthibitisha lugha ya kisheria ni kazi inayochukua muda mrefu kuliko vile ilivyodhaniwa hapo awali.

Kwa hivyo imeshauriwa kuachana na utaratibu wa kawaida wa kuthibitisha matamshi ya makubaliano kwa lugha zote zilizo rasmi kabla ya kutiwa saini.Lengo ni kuhakikisha kuwa makubaliano hayo ya mpito yataweza kutiwa saini mwaka huu.

Lakini mbali na tatizo la kutafsiriwa maelfu ya kurasa katika lugha 23,yadhihirika kuwa Kamisheni ya Ulaya ina wasiwasi mwingine pia.Kwani ina hofu kuwa baadhi ya nchi za ACP huenda zikabadilisha mawazo na zikaamua kutotia saini makubaliano ya mpito ya EPAs.

Wakati huo huo ni matumaini ya Kamisheni hiyo kuwa makubaliano hayo ya mpito yatatiwa saini na Baraza la Ulaya kabla ya nchi za Kiafrika,Karibea na Pasifiki kuamua vingine.

Ikiwa Baraza la Ulaya,linalojumuisha viongozi wa nchi au serikali za Umoja wa Ulaya pamoja na rais wa Kamisheni ya Ulaya,litaamua kutia saini makubaliano ya EPAs kama yalivyo, basi Shirika la Biashara Duniani WTO ndio litaweza kuarifiwa kuhusu mkataba huo.Baada ya kutiwa saini itakuwa vigumu mno kwa nchi za ACP kuyajadili upya makubaliano hayo.

Wakati huo huo,mwanaharakati anaegombea uchumi wa haki,Jean-Denis Crola wa tawi la Ufaransa la shirika la misaada OXFAM amesema,mapendekezo yaliyotolewa na Kamisheni ya Ulaya ni mkakati wa kuharakisha utaratibu wa kuidhinisha makubaliano ya mpito na hivyo kuziwajibisha nchi za ACP.

Mkakati huo lakini ni kinyume kabisa na utaratibu uliopendekezwa hivi karibuni na mbunge wa Ufaransa Christine Taubira anaeiwakilisha Guyana kuhusu EPAs. Katika ripoti iliyoamuriwa na Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy,kumeshauriwa mapendekezo yenye azma ya kurejesha imani katika mchakato wa majadiliano uliokumbwa na lawama za kutoaminiwa na pande zote yaani nchi za Umoja wa Ulaya na za ACP.

Ufaransa hivi sasa imeshika wadhifa wa urais wa Umoja wa Ulaya unaozunguka kila miezi sita.