1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waimarisha vikwazo vyake kwa Syria

24 Mei 2011

Vikwazo dhidi ya Syria, Iran, Libya na Belarus ni miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya walipokutana wa hiyo jana (23 Mei 2011) mjini Brussels, Ubelgiji.

https://p.dw.com/p/11Mmh
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine AshtonPicha: dapd

Sasa Umoja wa Ulaya umeamua kumuwekea Rais wa Syria, Bashar al-Assad, marufuku ya kusafiri na pia umemzuilia mali yake. Hatua hiyo imechukuliwa baada ya umoja huo kusita kwa muda mrefu kumlenga kiongozi huyo moja kwa moja.

"Rais wa Syria alifunguliwa njia ya kujiepusha na vikwazo hivyo kwa kurejea katika majadiliano ya kisiasa na kuacha kuwakandamiza wananchi wake mwenyewe. Lakini hakuitumia fursa hiyo. Kwa hivyo, hatuna budi kuimarisha vikwazo." Amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle anayehudhuria mkutano huo.

Mawaziri hao, wametoa mwito pia kuharakisha majadiliano ya amani ya Mashariki ya Kati na kuimarisha vikwazo dhidi ya Iran na Libya. Vile vile wamemkosoa Rais Ali Abdullah Saleh wa Yemen aliyekataa kutia saini makubaliano ya mpito.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido WesterwellePicha: DW-TV

Nayo Bahrain, imehimizwa kuendelea na mageuzi ya kisiasa. Kufuatia hotuba ya Rais Barack Obama wiki iliyopita, kuwa msingi wa kuundwa taifa lijalo la Palestina ni mipaka iliyokuwepo kabla ya vita vya mwaka 1967.

Umoja wa Ulaya unaamini wakati umewadia kuitisha mapema mkutano wa kundi la pande nne, kuhusu Mashariki ya Kati. Hata makubaliano ya amani ya hivi karibuni kati ya Wapalestina yanatia moyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Franco Frattini amesema, majadiliano hayo yafanywe upesi iwezekanavyo. Waziri mwenzake wa Ujerumani, Guido Westerwelle akaongezea kuwa wimbi la mageuzi linalopiga katika ulimwengu wa Kiarabu umesaidia pia mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati.

Hata hivyo mchakato wa amani unapaswa kusonga mbele ili kuhakikisha mafanikio ya kudumu kufuatia vuguvugu la mageuzi la hivi sasa.

Kwa upande mwingine, Umoja wa Ulaya unatofautiana katika suala la Libya. Baadhi ya nchi wanachama zinaunga mkono mashambulio ya NATO wakati zingine zikipinga.

Licha ya mashambulio ya miezi kadhaa, hakuna ishara ya waasi wa Libya kupata ushindi dhidi ya vikosi vya kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi.

Hata hivyo, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, alipofungua ofisi ya tume ya Umoja huo katika mji wa Benghazi ngome ya waasi wa Libya, alisema Umoja wa Ulaya upo tayari kutoa msaada kwa muda wowote watakaotaka wananchi wenyewe.

Hatimaye Umoja wa Ulaya unataka pia kulisaidia taifa jipya la Sudan ya Kusini litakaloundwa Julai mwaka huu, kufuatia kura ya maoni iliyopigwa mwezi wa Januari na wakaazi wa eneo hilo kuamua kujitenga na kaskazini. Umoja wa Ulaya upo tayari kutoa Euro milioni mia mbili ili kusaidia kujenga miundo mbinu na kupiga vita umasikini katika taifa hilo jipya.

Mwandishi: Christoph Hasselbach/ZPR
Tafsiri: Prema Martin
Mhariri: Josephat Charo