1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wakubali mpango wa kufufua uchumi

20 Machi 2009

Mjini Brussels,nchi wanachama katika Umoja wa Ulaya zimekubaliana kutoa Euro bilioni 5 ziada kutoka bajeti ya umoja huo kusaidia kufufua uchumi uliodorora.

https://p.dw.com/p/HG7B
German Chancellor Angela Merkel, center, puts her hands on the shoulders of French President Nicolas Sarkozy, left, and European Commission President Jose Manuel Barroso during a group photo at an EU summit in Brussels, Thursday March 19, 2009. European Union leaders open a summit Thursday fighting over a euro 5 billion recovery plan for new power grids and green energy and raising questions whether the hundreds of billions they are spending is enough to rescue their recession-hit economy. (AP Photo/Geert Vanden Wijngaert)
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel(kati)pamoja na Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy(kushoto) na Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso mjini Brussels.Picha: AP

Baada ya kuwa na mabishano ya miezi kadhaa,viongozi wa nchi na serikali kutoka nchi wanachama 27 wa umoja wa Ulaya hiyo jana mjini Brussels hawakupoteza muda kuukubali mpango mwengine kusaidia kunyanyua uchumi ulioathirika.Lakini sasa hakutokuwepo mipango mingine ya kitaifa.Kwani hadi sasa wanachama wa Umoja wa Ulaya kwa pamoja wameshatoa kiasi ya Euro bilioni 200 kusaidia uchumi ulioporomoka.Bilioni 200 zingine zimewekwa kando kwa ajili ya huduma za kijamii kama vile malipo ya wakosa ajira.Serikali za nchi hizo vile vile zimetumia Euro bilioni 300 kununua hisa za benki zilizokuwa na matatizo ya fedha.Isitoshe jumla ya Euro bilioni 2,500 zimewekwa kama dhamana kwa benki zilizokuwa hoi kifedha.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Czeki Mirek Topolanek ambae hivi sasa ameshika wadhifa wa urais katika Baraza la Umoja wa Ulaya amesema sasa ni kuongojea na kutazama iwapo hatua zilizochukuliwa zinasaidia kunyanyua uchumi.Kabla ya hapo hakuna fedha zaidi zitakazotolewa.Hiyo lakini ni kinyume na mwito wa Rais wa Marekani Barack Obama kuwa Umoja wa Ulaya utoe msaada zaidi kama sehemu ya jitahada za kimataifa kuzuia uchumi kuporomoka kote duniani.Wakati huo huo, viongozi wa Ulaya mjini Brussels wana mashaka yao kuhusu mpango wa Marekani wa kuchapisha noti na kuingiza kiasi cha Dola bilioni 1,000 katika masoko ya fedha.Wanadiplomasia mjini Brussels wanahofu kuwa hatua kama hiyo huenda ikashusha thamani ya sarafu.

Kuambatana na mpango uliokubaliwa siku ya Alkhamisi mjini Brussels,Euro bilioni 5 hasa zitatumiwa kwa miradi ya nishati na mawasiliano ya intanet. Fedha hizo zitatoka katika bajeti ya Umoja wa Ulaya na kutakuwepo usimamizi mkali.Baada ya makubaliano hayo kupatikana,Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso alisema:

"Nadhani hiyo ilikuwa muhimu na nimefurahi mno kuwa sasa nchi wanachama wameyakubali mapendekezo yaliyowasilishwa baada ya mkutano wa kilele wa Desemba ilyopita."

Viongozi wa Ulaya wamekubaliana kuwa na usimamizi mkali katika masoko ya fedha ya kimataifa na watawasilisha mapendekezo yao kwenye mkutano wa nchi 20 zilizoendelea kiviwanda na zinazoinukia kiuchumi G20-utakaofanywa London tarehe pili mwezi wa Aprili.Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema:

"Sisi tutahakikisha kuwa katika mkutano wa London kutapitishwa sheria za kudhibiti masoko ya fedha katika mfumo mpya.Na hapo tutashusghulikia kuwa na tume ya pamoja ya Ulaya kusimamia mfumo huo mpya."

Viongozi hao mjini Brussels wamekubaliana pia kuwasaidia wanachama walio na matatizo ya kifedha.Akiba ya msaada wa dharura wa Euro bilioni 25 utaongezwa kuwa Euro bilioni 50.Wanacahama wote wanapaswa kusaidiwa bila ya kujali ikiwa ipo Ulaya ya Mashariki au ya Magharibi. Kansela Merkel amesema kwanza kila mmoja anapaswa kujisaidia mwenyewe.Lakini msaada utatolewa kunapotokea dharura.

Mwandishi: B.Riegert/P.Martin/DPAE

Mhariri: O.Miraji