1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wakutana Bratislava kuijadili 'Brexit'

Mohammed Khelef16 Septemba 2016

Viongozi 27 wanakutana kwenye mkutano huu maalum wa kilele kuzindua mpango unaokusudiwa uidhinishwe mjini Rome mwezi Machi mwakani katika maadhimisho ya miaka 60 ya mkataba wa kuazishwa kwa Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/1K3Xf
Kutoka kushoto, Waziri Mkuu wa Denmark, Lars Lokke, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Charles Michel, kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Bratislava, Slovakia.
Kutoka kushoto, Waziri Mkuu wa Denmark, Lars Lokke, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Charles Michel, kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Bratislava, Slovakia.Picha: picture-alliance/dpa/O. Hoslet

Viongozi wote wakuu wa mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya, kasoro Uingereza, wanakutana mjini Bratislava, Slovakia, hivi leo (Ijumaa ya 16 Septemba), katika mkutano wa kilele ambao unalenga kuzungumzia mustakabali wao baada ya Uingereza kupiga kura ya kujitoa kwenye Umoja huo, sambamba na masuala ya ushirikiano wa ulinzi na usalama mipakani, wakijaribu kutibu majeraha ya mpasuko walionao kwenye kadhia ya wimbi la wahamiaji wanaoingia barani Ulaya.

Katika wakati ambapo bado Ulaya inajaribu kujitibu majeraha ya mzozo mkubwa kabisa wa wakimbizi tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia, mashambulizi ya kigaidi na mporomoko wa kiuchumi wa mwaka 2008, viongozi hawa wanatazamia kuwa wanaweza kujifunza kutokana na kura ya Uingereza kujiengua kutoka Umoja huo.

Akiwasili kwenye mkutano huo asubuhi ya leo, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, taifa ambalo linabeba dhamana kubwa kwenye Umoja wa Ulaya, amekiri kwamba huu utakuwa mkutano wenye mjadala mkali sana.

"Suala sio kutarajia suluhisho kwa matatizo yote ya Ulaya kwenye mkutano mmoja. Ingawa tupo kwenye hali ngumu sana, mkutano huu unahusiana na kuonesha kwa vitendo kwamba tunaweza kuwa bora zaidi kwenye maeneo ya usalama wa ndani na nje, vita dhidi ya ugaidi, ushirikiano wa kiulinzi." Kansela Merkel aliwaambia waandishi wa habari nje ya jengo la mkutano.

Katika mkesha wa mkutano huu wa kilele, Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk, aliwatolea wito viongozi wenzake kuwa wakweli kwa kila hali wanapolitathmini suala la kujitoa kwa Uingereza kwenye Umoja huo.

Mkutano wa kuambiana ukweli

Mwenyeji wa mkutano huo wa kilele, Waziri Mkuu wa Slovakia, Roberto Fico, amesema baada ya Uingereza kujiondoa na kutokana na athari ya uamuzi huo, umefika wakati wa kuangaliana machoni na kuambiana ukweli, akiongeza kuwa anaamini marais na mawaziri wakuu 27 watakuwa wakweli sana kwenye mjadala kuhusiana hali ya Umoja wa Ulaya katika kipindi hiki.

Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk.
Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk.Picha: Getty Images/AFP/M. Ericsson

Mbali na suala hilo la Uingereza, mjadala mzito pia unatazamiwa kwenye suala tete la wahamiaji. Akiwasili kwenye mkutano huo asubuhi hii, Waziri Mkuu wa Luxembourg, Xavier Bettel, ambaye wiki hii waziri wake wa mambo ya nje alizusha mzozo wa kidiplomasia kati ya nchi hiyo na Hungary kwa kupendekeza Hungary isitishwe au ifukuzwe moja kwa moja kwenye Umoja wa Ulaya kutokana na sera zake kuelekea wakimbizi, amesema anaamini kuwa baada ya yote hayo, Ulaya itaendelea kubakia moja.

"Unajuwa kuwa sisi ni familia moja, tuko pamoja kwenye familia hiyo. Ikiwa kuna matatizo kwenye familia, tunapaswa kujadili ndani ya familia na sio kumfukuza mtu. Hilo halitasaidia." Alisema waziri mkuu huyo wa Luxembourg.

Mwenzake wa Hungary, Viktor Orban, anayefahamika kwa misimamo mikali dhidi ya hoja ya mgawanyo wa wakimbizi miongoni mwa mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya, amesema asubuhi hii kwamba mataifa manne ya Ulaya ya Kati yatawasilisha mapendekezo ya pamoja ya utatuzi wa matatizo ya Umoja huo kwenye mkutano huu wa kilele.

Akizungumza na redio ya taifa ya nchi yake, Orban amesema anatarajia shinikizo la wakimbizi litaongezeka tena kwenye eneo la Balkan, mara tu hali ya hewa ikiwa mbaya na njia za baharini kuingia Italia zikawa ngumu kupitika.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AP/AFP
Mhariri: Saumu Yussuf