1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vurugu zazuka Palestina baada ya uamuzi wa Donald Trump

Amina Mjahid7 Desemba 2017

Watu 17 wamejeruhiwa kwa risasi na jeshi la Israel wakati Wapalestina walipoandamana katika Ukingo wa Magharibi na ukanda wa Gaza kupinga tamko la Rais wa Marekani Donald Trump kuitambua Jerusalem kama Mji Mkuu wa Israel

https://p.dw.com/p/2oy81
Gaza Protest gegen Trumps Entscheidung zu Jerusalem
Picha: Reuters/I. Abu Mustafa

Katika miji ya ukingo wa Mgharibi ya Hebron na Al Bireh maelfu ya waandamanaji walijitokeza huku wakisema kwa sauti kwamba Jerusalem ni mji mkuu wa Palestina. Kulingana na waliyoshuhudia baadhi ya waandamanaji waliwarushia mawe wanajeshi wa Israel.

Aidha mmoja ya waandamanaji alipigwa risasi ya moto huku wengine 14 wakilengwa kwa risasi za mpira, hii ikiwa ni kwa mujibu wa ripoti za madaktari. Na katika Ukanda wa Gaza nao waandamanaji walikusanyika karibu na mpaka wa Israel huku pia wakiwarushia mawe wanajeshi. Waandamanaji wawili walijeruhiwa huku mmoja akiwa katika hali mbaya.

Gazastreifen Protest gegen Donald Trump, US-Präsident - Anerkennung Jerusalem als Hauptstadt
Baadhi ya waandamanaji Palestina wakionyesha hisia zaoPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Hana

Awali mamlaka ya Palestina ilitoa wito wa kuwepo harakati za mapambano ya intifada kupinga tangazo la rais Trump kuitambua rasmi Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.

Palestina inataka mji mkuu wa taifa lao huru kuwa upande wa Mashariki ikiwa ni eneo lililonyakuliwa kwa mabavu na Israel mwaka wa 1967 wakati wa vita vya Mashariki ya kati na kuliunganisha eneo la Jerusalem na Israel hatua ambayo haijawahi kutambulika kimataifa.

Tillerson asema Trump  amezingatia matakwa ya raia wa Marekani katika uamuzi wake.

Huku hayo yakiarifiwa Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Rex Tillerson ameutetea uamuzi wa rais Trump na kusema kwamba kiongozi huyo wa taifa lililo na nguvu duniani amezingatia  matakwa ya raia wa Marekani katika uamuzi wake.

Tillerson yupo katika ziara ya siku tatu barani Ulaya lakini mazungumzo yake na washirika wa Marekani yamegubikwa na hisia mbali mbali zinazozidi kutolewa kufuatia tamko la rais Donald Trump.

USA Tillerson dementiert Rücktrittsgedanken
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex TillersonPicha: Reuters/Y. Gripas

Kwa upande wake Mkuu sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema uamuzi wa Marekani unatia wasiwasi na huenda ukalirejesha eneo la Mashariki ya kati kizani. Amesema hali ya Jerusalem inapaswa kuamuliwa na mataifa yote Israel na Palestina.

"Umoja wa Ulaya una nafasi ya wazi kabisa na ya pamoja. Tunaamini kuwa suluhu ya kweli ya mgogoro kati ya Israel na Palestina itaamuliwa na mataifahayo mawili na kwamba Jerusalem ni mji mkuu wa mataifa yote mawili Israel na Plaestina."

Urusi pia imepaza sauti yake juu ya uamuzi huo na kupitia msemaji wake Dmitry Peskov, imesema uamuzi wa Trump umeifanya hali kuwa ngumu zaidi Mashariki ya kati na kusababisha mgawanyiko katika jamii ya Kimataifa.

Waislamu kote duniani watolewa wito wa kupinga maamuzi ya Trump

Malaysian imeungana na mataifa mengine kuupinga uamuzi wa Trump. Waziri Mkuu wa nchi hiyo Najib Razak amewatolea wito waislamu kote duniani kupinga tamko la Trump la kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.

Ametoa wito kwa waislamu wote kupaza sauti zao na kuweka bayana kwamba wanaupinga uamuzi wa Trump.

Malaysia Premierminister Najib Razak
Waziri Mkuu wa Malaysia Najib RazakPicha: Getty Images/AFP/M. Vatsyayana

Juu ya hilo wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wametaka uitishwe  mkutano wa dharura kujadili uamuzi huo pamoja na hatua ya trump kuuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Telaviv hadi Jerusalem. 

Uswisi, Uingereza, Ufaransa, Bolivia, Misri, Italia, Senegal, na Uruguay Imetoa ombi hilo kwa raisi wa baraza hilo Japan kuandaa mkutano huo hapo kesho na kumtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kulihutubia baraza hilo.

Mwandishi Amina Abubakar/AFP/Reuters/AP/dpa

Mhariri:Yusuf Saumu