1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Mizozo ya eneo la Maziwa Makuu ipatiwe suluhisho

Grace Kabogo
25 Februari 2019

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa eneo la Maziwa Makuu, Said Djinnit, amezitaka nchi za ukanda huo kufanya juhudi ili kuleta suluhisho la kudumu katika eneo hilo linalokabiliwa na migogoro ya mara kwa mara.

https://p.dw.com/p/3E4Vt
Afrika Said Djinnit Sonderbeauftragter UN
Picha: Getty Images/AFP/J.D. Kannah

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Nairobi, Djinnit amesema eneo la Maziwa Makuu lina rasilimali chungu nzima ambazo zinaweza kuwasaidia sio tu raia wa mataifa hayo bali pia bara zima la Afrika kwa ujumla.

Mwanadiplomasia huyo, raia wa Algeria, ameyasema hayo katika awamu ya mwisho ya kuelekea kumaliza muhula wake rasmi kama mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ukanda wa Maziwa Makuu.

Amesema katika kipindi cha muda wa miaka minne iliyopita, kuna mafanikio kadha wa kadha ambayo yamefikiwa katika kuleta amani na maridhiano kwa mataifa ya ukanda huo licha ya changamoto zilizopo.

"Licha ya matatizo ya hapa na pale yanayoendelea katika ukanda huo eneo lote kwa ujumla limekuwa na hali ya amani. Kuna mikutano inayofanyika chini ya uongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC na Tume ya Umoja wa Afrika. Wanajaribu kuendeleza biashara na wanahimiza ushirikiano," alisema Djinnit.

Burundi Sicherheitskräfte Soldaten
Wanajeshi wa Burundi, moja ya nchi za eneo la Maziwa MakuuPicha: Getty Images/S. Platt

Kuhusu mivutano iliopo baina mataifa jirani na Kongo, mjumbe huyo amedokeza kuwa juhudi zinazoendeshwa chini ya mkataba maalum, nchi zilizo na mipaka na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo zinajaribu kuisaidia nchi hiyo kuleta amani ndani ya nchi, jambo ambalo litachangia katika kuimarisha amani kwenye kanda hiyo ya Maziwa Makuu. Hata hivyo, anahisi bado kuna hali ya kutoaminiana baina ya mataifa husika.

Juhudi zaidi zahitajika

"Kuna mafanikio lakini ningependelea kuona juhudi zaidi kukabiliana na tatizo hilo. Tumejaribu kuleta mjadala huo kweli unafanyika lakini bado hatuoni viongozi wakijitolea vile ambavyo tungependa kuona," alifafanua Djinnit.

Aidha amesema pana haja ya jumuiya ya kimataifa kuzidisha misaada kwa raia wa mataifa hayo na kuendeleza kampeni yake kutaka hali ya amani, usalama na ushirikiano kurejea katika maeneo hayo.

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa, amekuwa akiongoza jitihada za kushirikisha pamoja makundi yanayozozana kwa ushirikiano na viongozi wa ukanda mzima.

Kuhusu hali nchini Burundi, Djinnit amesema kuwa bado hali nchini humo ni ya kutia wasiwasi na akasisitiza umuhimu wa pande zote za mzozo wa Burundi zifikie makubaliano mara moja ili kuepukana na hali inayoweza kusababisha umwagikaji wa damu nchini humo.

Muhula wa Djinnit unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Machi ambapo nafasi yake itatwaliwa na mwanadiplomasia raia wa China, Huang Xia, kama mjumbe wake mpya katika eneo la Maziwa Makuu.

Mwandishi: Reuben Kyama/DW Nairobi
Mhariri: Mohammed Khelef