1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN SECURITY RESOLUTION

Aboubakary Jumaa Liongo17 Desemba 2008

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana limeidhinisha azimio la kuruhusu nchi zilizoamua kupambana na maharamia wa kisomali kuendesha harakati hizo ndani ya Somalia

https://p.dw.com/p/GHmF
Miongoni mwa maharamia wa kisomali wakiwa katika boti wanazotumia kuteka nyara meli kwenye nchi hiyoPicha: AP

Hatua hiyo ya Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa, imefuatia kuongezeka kwa vitendo vya utekaji nyara meli vinavyofanywa na maharamia wa kisomali katika pwani ya nchi hiyo ambayo ni njia muhimu kwa meli za mizigo.



Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitishwa kwa kauli moja azimio jipya kuruhusu kwa mwaka mmoja harakati za kimataifa dhidi ya maharamia hao wa kisomali kufanyika ndani ya nchi hiyo ya pembe ya Afrika iliyogubikwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu sasa.


Azimio hilo pamoja na mambo mengine linalaani na kutaka kuchukuliwa hatua dhidi ya maharamia hao na majambazi wanaoteka nyara meli katika pwani ya nchi hiyo.


Linatoa wito kwa nchi, jumuiya na mashirika ya kimataifa yenye uwezo wa kupambana na vitendo hivyo kushiriki kwa dhati katika harakati hizo dhidi ya maharamia


Aidha linayataka mataifa na wale watakaoshiriki katika harakati hizo, kuingia makubaliano rasmi na nchi zitakazokuwa tayari kuwachukua maharamia watakaokamatwa kwa ajili ya kufikishwa mbele ya sheria, hususani kwa nchi zilizo jirani na Somalia.


Imekuwa ikielezwa ya kwamba juhudi za kimataifa kupambana na maharamia hao zimeshindwa kuzaa matunda kutokana na vikosi vinavyohusika na harakati hizo kutokuwa na ruhusa ya kuendeleza mapambano hayo ndani ya Somalia kwenye ngome ya maharamia hao.


Hata hivyo azimio hilo halijafafanua ni aina gani ya majeshi yatakayoshiriki katika harakati hizo iwe za ardhini au angani na pia iwapo majeshi ya Marekani yatashiriki.


Kwa upande wake kamishna wa Umoja wa Afrika anayehusika na masuala ya amani na usalama Aramtane Lamamra alisema kuwa tatizo la maharamia hao limesababishwa na hali jumla ya kiusalama nchini Somalia nchi ambayo haina sheria kwa sasa.


Wakati huo huo maharamia hao wameteka nyara meli nne za kutoka China, Indonesia na Uturuki, mnamo wakati ambapo Kenya imeanza kufanya doria kali katika anga na pwani ya eneo lake na kutoa onyo kwa maharamia hao.