1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN wahimiza mbinu za kuzuia kuharibika kwa hali ya hewa

28 Novemba 2018

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa jukumu la kuilisha dunia yenye njaa inaendelea kuwa ngumu kwani mabadiliko ya hali ya hewa na kupungua kwa ardhi na rasilimali nyingine kunadhoofisha mifumo ya chakula.

https://p.dw.com/p/392kE
Klimawandel | Symbolbild
Picha: picture-alliance/dpa/ZB/P. Pleul

Ripoti hiyo ya Shirika la Chakula na Kilimo na Umoja wa Mataifa, FAO, iliyotolewa leo inaeleza kuwa kuongezeka kwa idadi ya watu kunahitaji upatikanaji mkubwa zaidi wa chakula bora kwa bei nafuu. Lakini kuongeza uzalishaji mashambani ni vigumu ikizingatiwa hali mbaya ya raslimali, kwani binadamu wamezidisha viwango vya kile ambacho ardhi inaweza kubeba kwa suala la ardhi, maji na mabadiliko ya hali ya hewa.

Upatikanaji chakula pia unahatarishwa na ugomvi wa kiraia pamoja na migogoro mingine. Nchini Yemen, ambapo maelefu ya raia wameuawa kutokana na mashambulizi ya angani yanayofanywa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, shirika la kimataifa la kuwasaidia watoto, Save the Children, limesema watoto elfu 85 chini ya umri wa miaka mitano huenda walifariki dunia kutokana na njaa au magonjwa kufuatia vita hivyo.

Klimawandel | Symbolbild
Picha: picture-alliance/pa/AP Photo/J. Amis

Kadhalika, Shirika la Mipango ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa imesema kwamba uzalishaji wa hewa chafu duniani uliongezeka tena mwaka 2017 baada ya miaka mitatu ya kusimamishwa, ikiashiria kwamba ni muhimu kwa mataifa kutekeleza Mkataba wa Kihistoria wa Paris wa kuiweka ongezeko la joto duniani chini ya nyuzi joto 2.

Mkuu wa shirika hilo, Satya Tripathi, amesema kuna ushahidi wa kutosha kwamba mataifa hayachukui hatua za kutosha kubadili hali hiyo.Satya amesema, "Kwa sasa tunaelekea nyuzi joto 3.2. Iwapo tunahitaji kuteremka hadi nyuzi joto mbili, tunafaa kuweka juhudi mara tatu. Iwapo tunataka kufikia nyuzi joto 1.5 tunafaa kuweka juhudi mara tano zaidi ya tunachokifanya kwa sasa. Kuna ushahidi wa kutosha wa kuaminika kuwa tunafaa kufanya vizuri kuafikia malengo yetu."

Hayo yakijiri, Tume ya Ulaya leo inazindua ripoti ya Muungano wa Ulaya ambayo inaeleza kuwa itapunguza uzalishaji wa hewa chafu hadi sufuri ifikapo mwaka 2050, ishara ya kuwepo kwa ajenda kuu ya hali ya hewa. Pendekezo hilo linajiri siku kadhaa kabla ya mkutano wa mataifa wanachama wa Mpango wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, utakaoanza Jumapili tarehe 2 Desemba, mjini Katowice, Poland.

Klimawandel | Symbolbild
Picha: picture-alliance/dpa/Geisler-Fotopress

Ripoti hiyo aidha imetoa mfululizo wa mapendekezo ikiwemo kuboresha hisa za makaazi, kupanua sekta ya nishati mbadala, kuimarisha umeme wa nishati mbadala ili kujitenga na mafuta yanayochafua mazingira na kubuni mtandao mzuri wa usafiri.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/APE/AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef