1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yaiwekea vikwazo Korea kaskazini

Sekione Kitojo
23 Desemba 2017

Kwa kuungwa mkono na China, baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinisha vikwazo vipya siku ya Ijumaa (22.12.2017) ambavyo vitaizuwia Korea Kaskazini kupata mahitaji ya muhimu kwa mpango wake wa kinyuklia.

https://p.dw.com/p/2prt5
UN-Sicherheitsrat in New York zu Situation in Nahost
Picha: Reuters/B. McDermid

Baraza  hilo kwa kauli  moja  liliidhinisha  azimio  lililotayarishwa  na  Marekani  ambalo pia  linaamuru  kurejeshwa kwa  wafanyakazi  wa  Korea  Kaskazini waliopelekwa  nje  ya  nchi  hiyo  kupata  mapato  ambayo  ni  kwa ajili  ya  utawala  wa  Kim Jong-Un.

Ni vikwazo vya  tatu  kuwekwa  dhidi  ya  Korea  kaskazini  mwaka huu  na  vinakuja  wakati Marekani  na  Korea  kaskazini  hazioneshi ishara  ya kuwa  tayari  kuanzisha  mazungumzo  juu  ya  kumaliza mzozo  huo  katika  rasi  ya  Korea. Rais  wa  Marekani Donald Trump  Ijumaa  liisifu hatua  hiyo, akisema  jumuiya  ya  kimataifa inataka  kuleta  amani  na  utawala  huo uliotengwa.

Nordkorea Diktator Kim Jong-un
Kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong UnPicha: picture-alliance/dpa/Yonhap/R. Sinmun

"Baraza  la  Usalama  la  Umoja  wa  Mataifa  lilipiga  kura  15-0 kuunga  mkono  vikwazo  vya  ziada  dhidi  ya  Korea  kaskazini. Dunia  inataka  amani , sio  kifo!" aliandika  Trump  katika  ukurasa wa  Twitter.

Azimio  hilo  linapiga  marufuku  upelekaji  wa  karibu asilimia 75 ya bidhaa za  mafuta  yaliyosafishwa  nchini  Korea  Kaskazini , kuweka ukomo katika  upelekaji  wa  mafuta  ghafi  na  kuwaamuru raia wote wa  Korea  kaskazini  wanaofanyakazi  nje  ya  nchi  kurejeshwa nyumbani  ifikapo  mwishoni  mwa  mwaka  2019.

Mswada wa  Marekani

Marekani iliwasilisha  mswada  wa  azimio  hilo siku  ya  Alhamis kufuatia  majadiliano  na  China, mshirika  mkubwa  wa  Korea kaskazini  na nchi  ambayo ndio inayosafirisha  mafuta  kwa  wingi nchini  humo.

USA UN-Sicherheitsrat Nikki Haley
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki HaleyPicha: Getty Images/D. Angerer

Akieelezea  Korea  Kaskazini  kama "mfano  mkubwa  wa  kusikitisha wa  uovu katika  dunia  ya  sasa," balozi  wa  Marekani  katika Umoja  wa  Mataifa  Nikki Haley  amesema  vikwazo  hivyo  vipya "vinaakisi hasira ya jumuiya ya kimataifa dhidi ya hatua za utawala wa Kim. Azimio  hilo " linatuma  ujumbe  wa  wazi kwa  Pyongyang kwamba  ukaidi  zaidi  utakaribisha  adhabu  zaidi  na  kutengwa," amesema  balozi  huyo.

Hatua  hizo  zinakuja  kutokana  na  majaribio  ya  Korea  ya Kaskazini  ya  makombora  ya  masafa  marefu  ICBM  hapo Novemba  28 ambapo  ilionekana  kuwa  ni  hatua  kubwa  iliyopigwa na  Korea  Kaskazini  katika  jaribio  lake  la  kuitishia  Marekani  kwa mashambulizi  ya  kinyuklia.

Nordkorea Raketenstart
Kombora la Korea kaskazini Picha: picture-alliance/dpa/Kcna

Trump  alitishia "kuivuruga  kabisa " Korea  Kaskazini  iwapo itaishambulia Marekani  wakati Korea  Kaskazini  inasisitiza  kwamba dunia lazima  ikubali  kwamba  nchi  hiyo  ni  moja  kati  ya  nchi zenye  silaha  za  kinyuklia.

Korea kaskazini yapunguziwa kuuziwa mafuta

Mwezi uliopita , Trump  alimtaka  rais  wa  China  Xi Jinping  kuacha kuipelekea  mafuta  Korea Kaskazini, hatua  ambayo ingedhoofisha uchumi  wa  nchi  hiyo  ambao  unamatatizo. Upelekaji  mafuta  ghafi umepunguzwa  hadi mapipa  milioni  nne kwa  mwaka  na  ukomo wa mapipa 500,000 ya bidhaa  za  mafuta  yaliyosafishwa, ikiwa  ni pamoja  na  dizeli  na  mafuta  ya  taa, yanayotarajiwa  kupelekwa mwakani, ni  chini kutoka  mapipa  milioni mbili katika vikwazo vilivyopita.

Liu Jieyi, chinesischer UN-Botschafter
Balozi wa China katika Umoja wa MataifaPicha: Kena Betancur/Getty Images

Iwapo Korea  Kaskazini  itafanya  jaribio  jingine  la  kinyuklia  ama majaribio  ya  makombora  ya  masafa  marefu ICBM, "baraza  la Usalama  litachukua  hatua  nyingine  kuzuwia  mauzo mengine  kwa nchi  hiyo ya  petroli," limeeleza  azimio  hilo.

Marekani  ililenga  hapo  awali  kutaka  kuwafukuza  katika  muda  wa mwaka  mmoja  mamia  kwa  maelfu  ya  wafanyakazi  wa  Korea Kaskazini, wengi  wao  wakifanyakazi  nchini  Urusi  na  China, lakini muda  huo  wa  mwisho ulirefushwa  hadi  miaka  miwili  baada  ya Urusi  kupinga.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Yusra Buwayhid