1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yasema watu milioni 20 wako katika hatari ya kufa njaa

Caro Robi
11 Machi 2017

Mratibu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na misaada ya kibinadamu amesema ulimwengu unakabiliwa na mzozo mkubwa zaidi wa kibinadamu tangu Umoja wa Mataifa kuundwa mwaka 1945.

https://p.dw.com/p/2Z0we
Hungersnot in Nigeria
Picha: picture alliance/dpa/Unicef/NOTIMEX

Stephen O'Brien ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa bila ya juhudi za pamoja na uratibu wa Jumuiya ya kimataifa kushughulikia baa la njaa, watu watakufa njaa na wengine wengi watataabika na kufa kutokana na magonjwa.

Umoja wa Mataifa unatoa wito wa kutolewa kwa michango ya fedha ili kuwepo kwa misaada ya dharura kuwasaidia raia wa Yemen, Sudan Kusini, Somalia na kaskazini mashariki mwa Nigeria na pia kuwepo njia salama kufikisha misaada katiak maeneo ya mizozo ili kuepusha janga.

O'Brien amesema wanahitaji dola bilioni 4.4 ifikapo mwezi Julai na kuongeza bila ya ufadhili huo, watoto watadumaa kutokana ana utapia mlo mbaya sana, hawataweza kwenda shuleni, kutakuwa na athari katika maendeleo ya kiuchumi na riziki,matumaini na vizazi vijavyo vitapotea.

Baa la njaa ndilo baya zaidi kushuhudiwa tangu 1945

Umoja wa mataifa na mashirika ya chakula yanaeleza baa la njaa kuwa pale asilimia 30 ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wanapokabiliwa na utapia mlo mbaya na idadi ya watoto wanaokufa ikiwa wawili au zaidi kati ya watu 10,000 kwa siku.

Jemen Unterernährung
Mwanamke aliyeathirika na njaa YemenPicha: Reuters/A. Zeyad

Nchini Yemen ambako kuna mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu, thuluthi mbili ya idadi ya wa Wayemen milioni 18.8 wanahitaji misaada na zaidi ya watu milioni saba wakikumbwa na njaa na hawajui pale mlo mwingine utakapotoka.

Idadi hiyo ni milioni tatu zaidi ya waathiriwa walioripotiwa mwezi Januari. Taifa hilo masikini zaidi la kiarabu linakumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe ambako watu 48,000 wameyatoroka mapigano katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Kwa mwaka huu, Umoja wa Mataifa unahitaji dola bilioni 2.1 kuwasaidia Wayemen milioni 12 kwa kuwapa misaada ya dharura. Ni asilimia 6 tu ya idadi hiyo ambayo mpaka sasa imepokea misaada. Katibu mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres anatarajiwa kufanya mkutano wa wafadhili kwa ajili ya Yemen tarehe 25 mwezi ujao mjini Geneva.

Guterres pia aliizuru Sudan Kusini taifa changa zaidi duniani linalokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka mitatu iliyopita ambako pia kuna janga kubwa la njaa. Zaidi ya watu milioni 7.4 nchini humo wanahitaji misaada.

Watoto ndiyo walioathirika zaidi

Zaidi ya watoto milioni moja wanakadiriwa kukumbwa na utapia mlo mkubwa wakiwemo watoto 270,000 ambao wako katika hatari ya kufa njaa iwapo misaada haitawafikia kwa wakati. Wakati huo huo mripuko wa kipindupindu katika maeneo kadhaa nchini humo yanaifanya hali kuwa mbaya zaidi. Mripuko huo ulianza mwezi Juni mwaka jana na umesambaa hivi sasa katika maeneo mengi.

Guterres UN PK zu Hungersnöte in Afrika
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: picture-alliance/Zumapress/A. Lohr-Jones

Somalia nako zaidi ya nusu ya idadi ya raia milioni 6.2 wanahitaji misaada ya kibinadamu wakiwemo watu milionii 2.9 ambao wanakumbwa na baa la njaa na hivyo wanahitaji misaada ya haraka ili kuyaokoa maisha yao.

Kaskazini mashariki mwa Nigeria, uasi wa miaka saba wa kundi la waasi la Boko Haram umesababisha vifo vya zaidi ya watu 20,000 na kupelekea wengine milioni 2.6 kuyahama makaazi yao.

Umoja wa Mataifa unasema utapia mlo ni mbaya sana katika eneo hilo kiasi cha kwamba watu wazima wamedhoofika sana kiasi cha kutoweza kutembea na baadhi ya jamiii zimepoteza watoto wao wote.

Mratibu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na misaada ya kibinadamu, ameonya pia watu milioni 2.7 nchini Kenya ambako kuna ukame mbaya hawana chakula cha kutosha na huenda idadi hiyo ikaongezeka hadi watu milioni 4 ifikapo mwezi ujao.

Mwandishi: Caro Robi/Ap/dpa

Mhariri: Sudi Mnette