1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ajali ya ndege ya Hammarskjold ilitokea 1961

20 Novemba 2015

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeidhinisha kwa kauli moja azimio linalozitaka nchi zote, kutoa taarifa zote zinazohusu ajali ya ndege ya mwaka 1961, iliyomuuawa katibu mkuu wa umoja huo, wakati huo Dag Hammarskjold.

https://p.dw.com/p/1H9ap
Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Dag Hammarskjöld
Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Dag HammarskjöldPicha: Imago

Mwezi Julai, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon aliliambia Baraza Kuu la umoja huo kwamba uchunguzi umegundua taarifa mpya inayoonyesha kuwa ndege hiyo ilishambuliwa ikiwa angani au uwezekano wa kuingiliwa kwa aina yoyote nyingine, hivyo wanataka uchunguzi zaidi ufanyike.

Dag Hammarskjold, aliyekuwa raia wa Sweden, alichaguliwa kama Katibu Mkuu wa pili wa Umoja wa Mataifa mwaka 1953, aliuawa pamoja na watu wengine 15, wakati akiwa njiani kuelekea katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ili kuwa mpatanishi katika kusimamisha mapigano kwenye jimbo la Katanga. Ndege yao ilianguka Rhodesia ya Kaskazini, ambayo kwa sasa ni Zambia.

Jopo la wajumbe watatu lililoteuliwa na Ban, limetoa wito wa kuwepo taarifa maalum kutoka Ubelgiji, Ufaransa, Ujerumani, Afrika Kusini, Marekani na Uingereza, katika kipindi cha miezi mitatu ya uchunguzi kuhusu ajali hiyo iliyotokea Septemba mwaka 1961. Jopo hilo limesema maswali yote hayakujibiwa ipasavyo.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 193 lilipitisha azimio linalozitaka nchi zote wanachama, hasa zile zilizoorodheshwa kwenye ripoti ya kurasa 99, kutoa taarifa sahihi walizonazo zinazohusiana na kifo cha Hammarskjold na kuziwasilisha kwa katibu mkuu.

Ban aliombwa kutea jopo la wataalamu

Baraza hilo lilimuomba Ban mwezi Disemba kuteua jopo huru la wataalamu watakaochunguza kifo hicho na kutoa taarifa mpya. Wataalamu hao ni kutoka Tanzania, Australia na Denmark.

Ripoti ya jopo hilo imeeleza kutokana na taarifa zilizotolewa na watu tisa walioshuhudia , walisaidia kubaini kwamba kulikuwa na ndege nyingine moja angani, wakati ndege ya Hammarskjold chapa DC-6 ilipokuwa inakaribia kutua katika uwanja wa ndege au ndege ya katibu mkuu huyo wa zamani, ilishika moto kabla haijafika ardhini au ililipuliwa na ndege nyingine wakati ikikaribia kutua Ndola.

Wachunguzi wakiangalia mabaki ya ndege hiyo
Wachunguzi wakiangalia mabaki ya ndege hiyoPicha: picture-alliance/dpa

Pia kulikuwa na taarifa mpya za ziada kwamba Wamarekani wawili, Charles Southall, kamanda wa zamani wa jeshi la maji la Marekani na Paul Abram, afisa wa zamani wa idara ya kikosi cha usalama cha anga, ambao huenda walisikiliza au walitafsiri matangazo ya redio usiku wa Septemba 17-18 mwaka 1961, ambayo wanaamini yalikuwa yakiripoti kuhusu shambulizi la ndege ya Hammarskjold ambayo ilichangia kuanguka kwake.

Jopo hilo limesema Uingereza imekataa kutoa mafaili yanayoonyesha shughuli za shirika la ujasusi la nchi hiyo katika eneo la Katanga. Jopo hilo limepata nyaraka za ushahidi kutoka taasisi ya utafiti wa bahari ya Afrika Kusini, zinazoonyesha kufanyika kwa ''operesheni Celeste'', kwa ajili ya kumuondoa Hammarskjold, kwa ushirikiano kutoka kwa mkurugenzti wa shirika la ujasusi la Marekani-CIA, Allen Dulles. Kwa mujibu wa jopo hilo, nyaraka hizo zilionyesha kuwa kiongozi huyo wa zamani wa Umoja wa Mataifa, angekuwa Leopoldville Septemba 12, mwaka 1961.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,AFPE
Mhariri:Yusuf Saumu