1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

UN yataka Waarabu waisaidie Syria

Jane Nyingi
6 Aprili 2017

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, linayataka mataifa ya Ghuba kujitolea zaidi kuwasaidia Wasyria ambao wamekimbia makwao kufuatia vita vilivyodumu kwa zaidi ya miaka sita.

https://p.dw.com/p/2aog3
Wakimbizi katika boti
Picha: picture-alliance/NurPhoto/A. Masiello

Akizungumza wakati wa ziara yake nchini Kuwait, ili kutia saini makubaliano ya msaada wa  dola milioni 10 kwa wakimbizi wa Syria walio nchini Iraq, Naibu Kamishna Mkuu wa UNHCR, Kelly T Clements, alisema hakuna matumaini yoyote  ya vita vya Syria kumalizimika karibuni. Clements  alisema ni jambo la kuhuzunisha kuwa idadi ya wakimbizi waliokimbia vita nchini Syria kufikia sasa ni zaidi ya millioni 5. Mkuu huyo wa shirika la UNHCR aliongeza kuwa hawajaona suluhisho lolote la kisiasa ili kuhakikisha raia wa Syria wanarejea nyumbani salama na kwa hiari.

Kupitia kwa msemaji wa shirika hilo la UNHCR, Babr Baloch, Clements alisema: "Tangu mwezi Februari mwaka huu, zaidi ya wakimbizi elfu 47 wamekimbia vita na uharibifu nchini Syria. Uturuki hivi sasa imewapatia makaazi karibu wakimbizi millioni tatu. Ndio maana UNHCR kwa mara nyingine tena  inaomba jumuiya ya kimataifa, mataifa wafadhili na hata watu binafsi kuyasadia mataifa kama Uturuki, Lebanon na mengine mengi  yaliyo eneo hilo, ambayo yameubeba mzigo wa wakimbizi kutoka Syria kwa muda mrefu."

Raia wa Syria wametafuta hifadhi nchini Uturuki, Lebanon, Jordan na Iraq tangu mwaka 2011yalipoanza  maandamano ya kuipinga serikali, ambayo yaligeuka na kuwa mgogoro kati ya waasi, wapiganaji wa kundi la IS, vikosi vya serikali na vile vinavyounga mkono na mataifa ya kigeni.

Watoto 500,000 Syria hawamo shuleni

Watoto wengi wanaishia kucheza mitaani kwakuwa shule zimebomolewa
Watoto wengi wanaishia kucheza mitaani kwakuwa shule zimebomolewa Picha: picture-alliance/AA/H. Nasar

Clements alisema kando na wakimbizi hao milioni 5 waliotafuta hifadhi nje ya Syria, kuna karibu watu millioni 13.5 walioachwa bila makao ndani ya Syria, na baadhi yao wamelazimika kuhama hama sio mara mbili, bali tatu au hata nne. "Hawa ni watu ambao hawawezi kuzisaidia familia zao, wanaishi  kwa hofu ya kushambuliwa kwa makombora, hawawezi kuwapeleka watoto wao shuleni," alisema Clements. Kwa mujibu wa takwimu za shirika la UNHCR, watoto millioni moja unusu ndani ya Syria hawamo shuleni.

Taifa la Kuwait ni mfadhili wa sita kwa ukubwa wa shirika la UNHCR, na kati ya mwaka 2013 na mwaka 2015 taifa hilo lilitoa msaada wa karibu  dola millioni 360. Naibu kamishna huyo wa shirka la UNHCR, alisema msaada waliopokea kutoka Urusi na Uchina ni mwingi ukiliganishwa na ule wa mataifa ya Ghuba japo yanajitahidi.

Mashambulio ya kemikali yajadiliwa

Wahudumu wa afya wa UN wanaochunguza Wasyria waliolengwa na shambulio la kemikali
Wahudumu wa afya wa UN wanaochunguza Wasyria waliolengwa na shambulio la kemikaliPicha: picture-alliance/AP Photo/DHA-Depo

Alipoulizwa iwapo wimbi la wakimbizi kutoka mataifa yanayokabiliwa na migogoro kama Syria, Iraq na Yemen linatazamiwa kupunguwa, Clements alijibu kwa ufupi kuwa ingawa matumaini ni kupatikana ufumbuzi wa kisiasa, lakini hali haionekani kuwa nzuri.

Wakati huo huo, Uingereza imejutia hatua ya kutochukua hatua mwaka 2013 kufuatia mashambulizi ya gesi nchini Syria licha ya kutishia kuwa matumizi ya silaha  za kemikali ni uvukaji mpaka. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Boris Johnson, alisema hayo wakati wa mkutano wa kimataifa kuhusu Syria ulioandaliwa na Umoja wa Ulaya mjini Brussels hapo Jumatano.

Mkutano huo hata hivyo uligubikwa na mashambulizi  ya silaha za kemikali katika mkoa wa Idlib nchini Syria mapema wiki hii ambalo kufikia sasa limesababisha vifo vya watu 72. Uingereza, Marekani na mataifa mengine duniani yameilaumu serikali ya Syria kwa kufanya mashambulizi hayo. Ikulu ya White House imeulaumu utawala wa awali wa  Barack Obama kwa kushindwa kuichukua hatua kali serikali ya Syria ili kuzuia mashambulizi kama hayo.

Mwandishi: Jane Nyingi/RTR/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef