1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yataka Wavenezuela kushiriki kura ya maoni

Lilian Mtono
14 Julai 2017

Umoja wa Mataifa umeitaka Venezuela kuwaacha raia kushiriki mchakato usio rasmi wa kura ya maoni ya kuhusu mabadiliko ya katiba Jumapili, na kuhakikisha vyombo vya usalama havitumii nguvu kubwa dhidi ya waandamanaji. 

https://p.dw.com/p/2gZVj
Venezuela - Krise
Picha: picture alliance/AP/A. Cubillos

 

Makundi ya upinzani yalitaka kufanyika kwa kura ya maoni baada ya miezi kadhaa ya maandamano, wakisema raia wa Venezuela wanatakiwa kuwa na kauli kuhusu mpango wa rais Nicolas Maduro wa kuandika upya katiba.

"Tunaziomba mamlaka kuheshimu matakwa ya wale wanaotaka kushiriki kwenye mchakato huu wa kura ya maoni na kuwahakikishia haki yao ya uhuru wa kujieleza, na kushiriki katika mikusanyiko ya amani," amesema msemaji wa masuala ya haki za binadamu wa umoja wa Mataifa, Liz Throssell, alipozungumza na waandishi wa habari mjini Geneva leo hii.

Mamia kwa maelfu ya watu waliandamana mitaani nchini Venezuela katika miezi ya hivi karibuni wakishinikiza kuondoka kwa Rais Nicolas Maduro madarakani, wakati taifa hilo likikabiliwa na upungufu wa chakula, kuanguka kwa thamani ya sarafu na mfumuko mkubwa wa bei. Takriban watu 100 walikufa na wengine 1,500 wakijeruhiwa kwenye machafuko ya kuipinga serikali yaliyoanza mwezi Aprili.

Venezuelas Präsident Nicolas Maduro
Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro anataka kuundwa kwa bunge la katibaPicha: Picture alliance/dpa/F. Batista/Prensa Miraflores

Maduro anaomba kuundwa kwa chombo kipya kitakachoitwa bunge la katiba litakalokuwa na mamlaka ya kuandika upya katiba na kuliondoa bunge la hivi sasa linalotawaliwa na upinzani kupitia kura itakayofanyika Julai 30.

Ofisi ya masuala ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imepokea madai kwamba baadhi ya wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama walitumia mbinu za kuharibu, kutishia na kuongeza hofu katika kujaribu kuwazuia watu kuandamana, amesema Throssell.

Wakati mzozo nchini humo ukifikia hatua mbaya na Maduro akikabiliwa na upinzani mkali kwa kile ambacho wakosoaji wake wanasema ni hatua za kiimla, shirika la kimataifa la wakimbizi, UNHCR limeonya kwamba idadi ya maombi ya hifadhi   kutoka nchini humo imeongezeka.

Mwaka jana, kulikuwa na takriban raia wa Venezuela 27,000 walioomba hifadhi duniani kote. Kwa mwaka huu wa 2017, zaidi ya raia 52,000 waliomba hifadhi, limesema shirika hilo kwenye taarifa yake.

Marekani, Brazil na Argentina zinaongoza kwa kupokea waomba ya hifadhi kutoka Venezuela, kulingana na UNHCR.

Shirika hilo limerejea mwito wake kwa mataifa kulinda haki za raia wa Venezuela, hususan haki ya kuomba hifadhi pamoja na kupatiwa huduma zenye ufanisi wanaposhughulikiwa maombi yao ya hifadhi, alisema, Throssell.

Mwandishi: Lilian Mtono/Rtre/Afpe.

Mhariri: Gakuba, Daniel