1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yauomba ulimwengu utoe michango ya dharura kwa Pembe ya Afrika

25 Julai 2011

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, limeutolea wito ulimwengu mzima kufanya kila linalowezekana kuchukua hatua za kuliokoa eneo la Pembe ya Afrika linalokumbwa na baa kubwa la njaa na ukame.

https://p.dw.com/p/1234X
Jacques Diouf,Mkurugenzi mkuu wa FAOPicha: AP


Kauli hizo zimetolewa katika kikao cha dharura cha FAO kilichoandaliwa mahsusi kwasababu ya tatizo hilo. Kulingana na takwimu rasmi, kiasi ya Wasomali milioni 3.7 wanakabiliwa na kitisho cha njaa. Ifahamike kuwa njaa ukame umeliathiri eneo la Pembe ya Afrika zikiwemo nchi za Ethiopia na Kenya.

Hali ni mbaya

Akizungumza katika ufunguzi rasmi wa kikao hicho cha dharura, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula, FAO, Jacques Diouf, alisema kuwa hali ni mbaya na hatua za dharura zinahitajika ili kuwanusuru wakaazi wa eneo hilo la Pembe ya Afrika.

Mapema  mwezi huu, Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi kuwa maeneo mawili ya Somalia yanakabiliwa na njaa. Ifahamike kuwa maeneo hayo yanayodhibitiwa na wapiganaji wa Al Shabaab wanaoaminika kuwa na mafungamano na kundi la kigaidi la Al Qaeda. Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Somalia aliye pia Waziri wa Mambo ya Nje alikihudhuria kikao cha leo, Mohamud Ibrahim anaelezea kuwa, " Wasomali wanakabiliwa na njaa kwasababu kadhaa ikiwemo mvua chache kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, harakati za kundi la Al Shabaab zilizoweka amri ya kuyazuia mashirika ya msaada kusambaza vyakula, pamoja na usalama duni katika eneo hili."

Flash-Galerie Dürre ohne Ende Menschen in Äthiopien von Dürre und Hunger bedroht
Mtoto wa Ethiopia anayekabiliwa na Utapia mlo sugu.Picha: picture-alliance/dpa

Mifuko ya Chakula

Wakati huohuo, katika kikao hicho hicho Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa, WFP, umetangaza pia kuwa shirika hilo litaanza kudondosha kwa ndege mifuko ya chakula cha msaada. Shughuli hiyo imepangwa kuanza hapo kesho katika mji wa Mogadishu pamoja na eneo la mashariki mwa Ethiopia na eneo la Kaskazini mwa Kenya linalopakana na Somalia. Itakumbukwa kuwa mkurugenzi mkuu wa WFP, Josette Sheeran aliizuru Mogadishu wiki iliyopita na akiwa mkutanoni hii leo alitahadharisha kuwa hali ni mbaya sana na kwamba, " Janga hili linaweka bayana kuhusu umuhimu wa kuwa na ushirikiano katika nyanja za kimataifa, kitaifa na kikanda ili kuuimarisha uwezo wa kuhakikisha kuwa chakula kinatosha kwa minajili ya kulipiga vita tatizo la njaa na utapia mlo.Naamini hilo linawezeka. Kwa sasa hali ni mbaya sana." 

Kitisho na michango

Duru zinaeleza kuwa hali hii ya ukame haijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 60. Kwa sasa, Umoja wa Mataifa tayari umepokea kiasi ya euro milioni 696 tangu iwasilishe rasmi  mwezi Novemba mwaka uliopita ombi la mchango. Hata hivyo kiasi ya euro bilioni moja nyengine zinahitajika ifikapo mwishoni mwa mwaka ili kukabiliana na hali ya dharura  iliyopo.

Hunger in Somalia Afrika
Wanawake wa Kisomali wakisubiri chakula MogadishuPicha: picture-alliance/dpa

Benki ya Dunia hii leo imeahidi kutoa kiasi ya euro milioni 500 ambazo zitatumika kuifadhili miradi ya ufugaji na kiasi ya euro milioni 12 kati ya hizo zitatumiwa kununua bidhaa za msaada kwa wanaokufa njaa.

Ili kuzipa msukumo harakati hizo, Waziri wa Kilimo wa Ufaransa, Bruno Le Maire alisema kuwa mataifa wahisani watakutana mjini Nairobi siku ya Jumatano ili kulijadili tena suala la njaa.

Mwandishi: Mwadzaya, thelma-AFPE/DPAE/ FAO-Multimedia

Mhariri:Yusuf Saumu