1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Unesco na mkutano wa kila mwaka kuyateua maeneo

Nijimbere, Gregoire2 Julai 2008

Mkutano mkuu wa kila mwaka wa Shirika la Umoja wa mataifa kwa ajili ya elimu, sayansi na utamaduni Unesco wa kuyateua maeneo muhimu ya kitamaduni na ya kiasili na ambayo ni budi yahifadhiwe, umeanza jana nchini Canada.

https://p.dw.com/p/EV33
Wajumbe mkutanoni Unesco ikiadhimisha miaka 60 tangu iundwe katika sherehe mjini Paris 2005Picha: Montage/dpa

Kamati ya rasili mali za kuhifadhiwa za Shirika la Umoja wa mataifa kwa ajili ya elimu, sayansi na utamaduni Unesco ambayo imeundwa na wataalamu, inakutana mjini Montreal katika jimbo la Quebec nchini Canada hadi tarehe 10 mwezi huu. Kwa muda wa wiki mmoja na nusu, wataalamu hao wa Unesco watateua maeneo yanayostahili kuorodheshwa miongoni mwa maeneo yanayokubalika duniani kwamba ni yenye thamani maalum kitamaduni au kiasili.

Maeneo yatakayoteuliwa yatakuja kurefusha orodha ya maneo 851 yaliyotengwa katika nchi 141 ambapo maeneo 766 ni ya kitamaduni na mengine 25 ya kiasili.

Mwaka huu kuna mapendekezo kutoka nchi 41 zikiwemo zile zinazopendekeza kwa mara ya kwanza kama Kirghizstan kuhusu mlima mtakatifu wa Sulamain-Too, kituo cha zamani cha kilimo cha Kuk katika Papouasie Nouvelle Guinée na kituo cha maonyesho ya vitu vya kale cha Al-Hijr nchini saudi Arabia.

Kwa jumla vituo 34 vya kitamaduni vitapendekezwa. Vituo hivyo ni pamoja na eneo la kitamaduni la Buenos Aires mji mkuu wa Argentina, vijiji mtindo wa kisasa mjini Berlin Ujerumani, njia ya leri kutoka Kalka hadi Shimla nchini India pamoja na yile kutoka Albula nchini Usuisi hadi Bernina nchini Italy, majengo ya kanisa ya kiarmenia nchini Iran, maeneo matakatifu ya baha's mjini Haifa nchini Israel, kanisa la Leo nchini Nicaragua. Miongoni mwa maeneo sanifu kiasili ni pamoja na miporomoko ya maji kwenye milima ya Joggins nchini Canada, eneo la wanyama pori la kitalii la Sangingshan nchini China, tambarare la ziwa Hovsgol katika mkoa wa Mongolia nchini China vile vile. Ufaransa itapendekeza eneo la kiasili la Nouvelle-Caledonie katika bahari kuu ya Hindi na sehemu 14 zilizojengwa na mhandisi wa mfalme Louis wa 14. Barani Afrika, Kenya itapendekeza misitu mitakatifu ya Mijikenda Kaya kwenye pwani ya bahari kuu ya Hindi wakati Mauritius ikitetea eneo lake la kitamaduni lililotengwa la Morne.

Kama utaratibu wake, wajumbe wa Shirika la Umoja wa mataifa kwa ajili ya elimu, sayansi na utamaduni Unesco, huyatembelea kabla maeneo hayo yanayopendekezwa na kukadiria thamani yao kitamaduni au kiasili na mipango ya uhasibu wa vituo au maeneo hayo kutoka kwa viongozi. Wataalamu hao huwasilisha ripoti yao kabla ya mkutano wa kuyateua maneo.

Kiasi ya maeneo 30 huteuliwa kila mwaka, mfumo ulionzishwa na Taarifa ya Unesco ya mwaka 1972 kwa ajili ya ulinzi wa maeneo maalum duniani.

Mbali na kuyateua maeneo mapya, mkutano huo wa sasa nchini Canada, unatarajia pia kuamua juu ya hatima ya maeneo yaliyoteuliwa tayari na ambayo yanakabiliwa na hatari ya kutoweka kutokana na ujenzi. Maeneo hayo ni pamoja na kituo cha tambarare la mto Elbe huko Dresde nchini Ujerumani ambapo mwaka mmoja uliopita viongozi walipata onyo kutoka kwa Unesco juu ya ujenzi wa daraja kubwa la mita 600 mjini kati. Kituo kingine ni mji wa Islambul nchini Uturuki ambao uliorodheshwa mwaka 1985 miongoni mwa maeneo maalum ya kitamaduni duniani na ambao sasa unakabiliwa na ujenzi kiholela. Mwaka uliopita Shirika hilo la Unesco lilifuta kwenye orodha yake eneo la Oryx ya kiarabu ya Sultani ya Oman baada ya viongozi kulipunguza eneo hilo.