1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNHRC yataka wakuu wa kijeshi Myanmar washtakiwe

John Juma DPAE/RTRE
18 Septemba 2018

Wanadiplomasia wametoa kauli zao kuhusu ripoti ya uchunguzi iliyosema takriban watu 10,000 waliuawa na zaidi ya makaazi 37,000 ya watu kuharibiwa, baada ya walinda usalama wa Myanmar kushambulia jamii ndogo ya Warohingya

https://p.dw.com/p/356pC
Schweitz Marzuki Darusman Bericht zu Myanmar PK in Genf
Picha: Reuters/D. Balibouse

Shirika la haki za binadaamu la Umoja wa Mataifa, linastahili kukusanya ushahidi dhidi ya watuhumiwa waliofanya maovu nchini Myanmar ili ushahidi huo utumiwe na waendesha mashtaka. Hayo yameelezwa Jumanne na nchi za magharibi na za Kiislamu.

Katika kikao cha shirika hilo la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, wanadiplomasia wametoa kauli zao kuhusu ripoti ya uchunguzi uliofanywa na umoja huo iliyosema takriban watu 10,000 waliuawa na zaidi ya makaazi 37,000 ya watu kuharibiwa, baada ya walinda usalama wa Myanmar kushambulia jamii ndogo ya Waislamu, Warohingya mnamo Agosti 2017.

Ripoti hiyo iliyotangazwa mwezi uliopita, iliwahusisha viongozi wakuu wa jeshi la Myanmar na mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya ubinadamu ikiwemo ubakaji, utesaji na utumwa.

Ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu?

Marzuk Darusman ambaye aliongoza ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika uchunguzi dhidi ya Myanmar, amesema ni vigumu kutafakari kiwango cha ukatili kilichofanywa na jeshi la Myanmar, Tatmadaw. Ameongeza kuwa ni ukosefu kabisa wa kuzingatia uhai wa raia.

Kwenye taarifa ya pamoja kwa baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binaadamu, nchi hizo zimependekeza kubuniwe jopo jingine lenye wajibu wa kukusanya, kujumuisha na kutathmini ushahidi ili kutayarisha mashtaka.

Ripoti ya uchunguzi yasema takriban Warohingya 10,000 waliuawa na makaazi 37,000 ya watu wa jamii ya Rohingya kuharibiwa pale walinda usalama wa Myanmar waliposhambulia jjimbo la Rakhine.
Ripoti ya uchunguzi yasema takriban Warohingya 10,000 waliuawa na makaazi 37,000 ya watu wa jamii ya Rohingya kuharibiwa pale walinda usalama wa Myanmar waliposhambulia jjimbo la Rakhine.Picha: picture-alliance/abaca

Mahakama ya kimataifa ya jinai iliyoko mjini The Hague, ilisema mwezi huu kuwa ina wajibu kisheria kuchunguza uhamiaji wa watu 700,000 wa jamii ya Rohingya kutoka Myanmar kuelekea Bangladesh, pamoja na visa vingine vya ukiukaji wa ubinadamu.

Myanmar yapinga ripoti ya uchunguzi

Lakini serikali ya Myanmar imeipinga ripoti hiyo na kusema jumuiya ya kimataifa inatoa madai y auwongo. Jeshi halikutoa kauli yake na shirika la habari la Reuters halikuweza kuwafikia Majenerali waliotajwa kwenye ripoti hiyo.

Balozi wa Myanmar katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Kyaw Moe Tun ameipinga ripoti hiyo akisema imeegemea upande mmoja huku akiongeza kuwa serikali yake haitambui jukumu lake.

Amekiambia kikao kuwa ripoti hiyo si hatari tu kwa mshikamano wa kijamii katika jimbo la Rakhine bali pia inahujumu juhudi za serikali kuleta amani, maridhiano y akitaifa na maendeleo katika nchi nzima.

Jumuiya ya Ushirikiano  ya nchi za  Kiislamu imesema yaliyogunduliwa kwenye ripoti ya mwisho ya uchunguzi kuhusu Myanmar, yanasikitisha na kuvunja moyo, na imeutaka Umoja wa Mataifa kuhifadhi ushahidi ili uweze kutumiwa mahakamani.

Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu linatarajiwa kuamua kuhusu mapendekezo hayo mwishoni mwa mwezi huu wa Septemba.

 

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman