1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upande wa upinzani Pakistan wasaka msimamo wa pamoja

Oummilkheir6 Desemba 2007

Nawaz Shariff na Benazir Bhuto wamtumia madai rais Musharaff uchaguzi uwe huru na wa haki.

https://p.dw.com/p/CY3S
Kiongozi wa upinzani Nawaz ShariffPicha: AP

Vyama vya upinzani vya Pakistan vinajaribu kusaka msimamo wa pamoja katika madai ya kutaka warejeshwe kazini majaji waliofukuzwa na rais Pervez Musharraf sheria ya hali ya hatari ilipotangazwa November tatu iliyopita.

Mawaziri wakuu 2 wa zamani,Benazir Bhuto na Nawaz Shariff,wote wawili wakiwa wamerejeas nyumbani hivi karibuni kutoka uhamishoni na wakuu wa vyama vikuu vya upinzani,wamesema watamtumia rais Pervez Musharraf “orodha ya madai” kwa lengo la kupata hakikisho kwamba uchaguzi wa bunge utakaoitishwa January nane ijayo, utakua huru na wa haki.

Viongozi hao wawili wa upinzani wanatishia kuususia uchaguzi huo ikiwa madai yao hayatazingatiwa.

“Maamuzi mengi yamepitishwa kwa ridhaa.Vipengee vya mwisho mwisho vitasawazishwa hii leo.Ni duru ya mwisho ya mazungumzo na orodha yetu itakamilishwa hii leo”-amesema hayo Ahsan Iqbal,msemaji wa chama cha Muslim League-PML- kinachoongozwa na Nawaz Shariff.

“Tumekubaliana kusahau hitilafu zetu za maoni na kuendeleza juhudi za pamoja kuhakikisha uchaguzi unakua huru na wa haki”ameongeza kusema Ahsan Iqbal bila ya kutoa maelezo zaidi.

Kwa mujibu wa mshiriki mwengine wa mazungumzo hayo,vyama vya Nawaz Shariff na Benazir Bhutto,PML na PPP vinajaribu kuijongeza misimamo yao kuhusiana na suala la kurejeshwa kazini majaji 37 waliofukuzwa na rais Pervez Musharraf baada ya kutangaza sheria ya hali ya hatari,November tatu iliyopita.

“Nnaamini tunaweza kuafikiana”-ameongeza kusema msemaji wa chama cha PML.

Benazir Bhutto,aliyerejea nyumbani kutoka uhamishoni,October iliyopita,amesema chama chake kina shaka shaka kama washiriki katika uchaguzi wa bunge mwezi ujao.Hata hivyo ameshatangaza muongozo wa chama chake na kuanza pia kampeni za uchaguzi tangu wiki iliyopita.

Benazir Bhutto anahisi suala la majaji linabidi litatuliwe na bunge jipya.Kwa upande wake Nawaz Shariff,aliyerejea Pakistan mwezi uliopita,ametoa mwito uchaguzi ususiwe ikiwa majaji hao hawatarejeshwa kazini.

Alituma hata hivyo maombi ya kutetea uchaguzi wa bunge ambayo yamekataliwa kutokana na ile hali kwamba aliwahi kuhukumiwa baada ya mapibnduzi ya mwaka 1999 yaliyomleta madarakani Pervez Musharaff.

Jenerali huyu wa zamani,aliyeapishwa kama rais wa kiraia wiki iliyopita-ameahidi kubatilisha sheria ya hali ya hatari,ikiitika madai ya upande wa upinzani na nchi za Magharibi.

Ameondowa lakini uwezekano wa kuwarejesha tena kazini majaji aliyowatimua,ikiwa ni pamoja na Iftikhar Chaudry,aliyewahi kua mweyekiti wa korti kuu .

Nawaz Shariff amepanga kukutana na Chaudry na baadae na mabalozi wan chi za kiislam mjini Islamabad.Haijulikani lakini kama viongozi wa serikali ya Pakistan watamruhusu Nawaz Shariff akutane na jaji huyo anaetumikia kifungo cha nyumbani.