1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani DRC wapinga mfumo wa kielektroniki katika uchaguzi

12 Aprili 2018

Vyama vitano vya upinzani vimesema vinatiwa wasiwasi mkubwa kuhusu jinsi tume ya uchaguzi nchini Congo CENI inavyojiendesha katika njia ya kiholela kuhusiana na usimamizi wa mchakato wa uchaguzi

https://p.dw.com/p/2vuWF
Demokratische Republik Kongo Wahl Wahlen Stimmtzettel Kinshasa
Picha: picture alliance/dpa

Vyama vya upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vimepinga vikali matumizi ya mfumo wa kieletroniki katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa mwezi Desemba mwaka huu. Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa jana mjini Kinshasa, vyama vitano vya upinzani vimesema vinatiwa wasiwasi mkubwa kuhusu jinsi tume ya uchaguzi nchini Congo CENI inavyojiendesha katika njia ya kiholela kuhusiana na usimamizi wa mchakato wa uchaguzi.

Vyama hivyo vimesisitiza vinapinga matumizi ya vifaa vya kieletroniki kutoka Korea Kusini katika uchaguzi ujao. CENI kwa upande wake inasisitiza ni muhimu katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa njia sahihi. Hata hivyo maafisa wa Korea Kusini siku ya Jumanne walijitenga na kampuni inayotengeza mashine hizo ikisema haiwezi kutoa hakikisho kama zitatumika ipasavyo.

Uchaguzi uliochelewesha nchini humo unatarajiwa kufanyika tarehe 23 Desemba kumchagua mrithi wa Rais Joseph Kabila ambaye mpaka sasa hajatangaza kama anaondoka madarakani au atajaribu kugombea urais licha ya katiba kutomruhusu kuwania muhula wa tatu.