1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani wadai Uganda yatuma jeshi Kenya

14 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CpAH

NAIROBI

Upinzani nchini Kenya umedai hapo jana kwamba Uganda imetuma majeshi katika mkoa wa magharibi wa nchi hiyo kufuatia ombi la serikali kabla ya kufanyika kwa maandamano yaliopangwa wiki hii dhidi ya serikali madai ambayo polisi imeyakanusha vikali.

Chama cha upinzani cha ODM kimesema wanakijiji wamewaona wanajeshi wakiwasili kwenye fukwe za Ziwa Viktoria na wengine wakivuka wakiwa ndani ya mabasi kwenye mpaka wa Malaba nchini Kenya.

Madai ya kutumwa kwa wanajeshi hao wa Uganda yanakuja siku chache kabla ya kuanza kwa maandamano hayo ya upinzani hapo Jumaatano.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga anagoma kutambuwa kuchaguliwa upya kwa Rais Mwai Kibaki au kuzungumza naye hadi hapo atakapokiri kwamba uchaguzi ulikuwa wa udanganyifu.

Odinga anasema iwapo atakutana na Kibaki kwa sababu ni rafiki yake atamwambia ameshindwa uchaguzi na kwamba anatakiwa awache urithi katika nchi hiyo na kwa vile amekuwepo kwa muda mrefu awache urithi wa kiungwana wa mtu alieshindwa uchaguzi na an’gatuke kwa madaha.

Makamo wa Rais wa Kenya Kalonzo Musyoka ambaye hadi wiki iliopita alikuwa akiongoza chama kidogo cha upinzani ameonya kwamba waandalizi wa maandamano ya wiki hii watawajibika kwa matokeo yake iwapo hawatoyafuta maandamano hayo.