1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani waongoza Zambia

31 Oktoba 2008

Kiongozi wa Upinzani Michael Sata aongoza uchaguzi wa Rais Zambia.

https://p.dw.com/p/Fl3b

Wazambia wamepiga kura jana kumchagua rais mpya kujaza pengo lililoachwa na kifo cha rais Levy Mwanawasa miezi 2 iliopita.Ingawa taarifa za hivi punde zinasema kiongozi wa Upinzani Michael Sata anaongoza kwa muujibu wa matokeo ya awali kutoka wilaya 13 za uchaguzi,Upinzani umeshatoa kilio kuwa mizengwe na udanganyifu imepita katika uchaguzi huu.Aliepigiwa upatu kushinda uchaguzi huu ni makamo-rais Rupiah Banda ambae aliiahidi kufanyika kwa uchaguzi huru na bila mizengwe.

Kiongozi wa Upinzani Michael Sata anaeongoza chama cha Patriotic Front, amekusanya hadi sasa kura 187,863 kwa 96,325 za makamo-rais Banda.Hii ni kwa muujibu wa maafisa wa Tume ya Uchaguzi.Hesabu hiyo imeegemea kuhesabiwa kwa wilaya 19 kati ya 150 za uchaguzi.

Sata anaedai kuwapigania masikini nchini ,alishindwa katika uchaguzi uliopita 2006 kwa marehemu Mwanawasa.

Shirika huru linalochunguza uchaguzi huu unavyokwenda la Zambia,limearifu mapema hii leo kwamba kwa jumla, uchaguzi ulipita kwa amani lakini, kumekuwapo visa kidogo visivyo vya kawaida katika uchaguzi.

Uchunguzi pekee wa maoni uliochapishwa na shirika la African market information group Steadman, umeonesha kiongozi wa Upinzani Bw.Sata akiongoza kwa 46% kwa 32% za mpinzani wake makamo-rais Banda.

Bw.Banda anatumai hatahivyo, kunufaika na hali ya kustawi kwa uchumi wa Zambia pamoja na umaarufu mkubwa wa marehemu Mwanawasa.Uchumi wa Zambia unaotegemea madini ya shaba umekua kwa kima cha wastani cha 5% kila mwaka tangu 2002 kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa katika masoko ya dunia.

Kiongozi wa upinzani Michael Sata alilituhumu jeshi na polisi kuwatisha wapiga kura.Na matamshi aliotoa mkuu wa majeshi -adai Michael Sata-yakibainisha kwamba uchaguzi tayari umefanyiwa mizengwe.Kutokana na hali hii,kiongozi wa upinzani adai hataridhia kushindwa.

Mkuu wa majeshi jamadari Chisuzi alionya katika TV pasizuke fujo na uchokozi na kwamba vyombo vya usalama viko macho. Wafuasi wa upinzani wamelitafsiri onyo hilo kama changamoto ya kuwapiga vita .

Makamo-rais Banda anadai kwamba mpinazni wake Sata angeshinda tu uchaguzi huu ikiwa ameungwamkono na wakaazi wa mashambani.

Sata anaungwamkono zaidi na wafanyikazi wa mijini.Ni maarufu kwa kutoa ahadi na matamshi ya kuwavutia wapigakura.Kwa mfano, katika kampeni yake ,mjumbe huyo wa zamani wa kibalozi akipigania kuteremshwa kodi za mapato na kuwapatia wazambia sehemu yao katika makampuni ya kigeni yaliopo Zambia.

Akiwa na umri wa miaka 71, Sata anagombea wadhifa huu wa urais kwa mara ya tatu baada ya kuangushwa mara mbili na Mwanawasa.

Mchambuzi wa kisiasa nchini Zambia Azuel Banda hatoi pongezi kwa somo yake makamo-rais Rupiah Banda:

"Tatizo kubwa la Rupiah Banda ni kuwa, hana mpango wake binafsi na hadi sasa hauingwimkono sana na chama chake tawala MMD.Bado yeye ni mapya na itavutia kuona itavyokua...."

Milolongo mirefu ya wapigakura hapo jana katika vituo 6.500 vya uchaguzi imebainisha shauku kubwa katika uchaguzi huu.Nani mwishoe, atatangazwa mshindi,ni swali la kusubiri kuona,kwani kutangulia katika chaguzi za Afrika si kufika.