1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani wasema unakaribia kuchukua madaraka Zimbabwe

Charo, Josephat2 Aprili 2008

Miito yatolewa kutaka matokeo rasmi ya mwisho yatangazwe

https://p.dw.com/p/DYzc
Wazimbabwe wakifuatilia matokeo kwenye televisheni ya taifa mjini HararePicha: AP

Upinzani nchini Zimbabwe umesema unakaribia kuchukua uongozi baada ya kupuuza tetesi kwamba utafanya mazungumzo ya kuondoka madarakani kwa rais Robert Mugabe.

Kiongozi wa upinzani, Morgan Tsvangirai na viongozi wa serikali ya Mugabe wamekanusha ripoti za vyombo vya habari kwamba mkataba umefikiwa kuandaa kuondoka kwa Mugabe madarakani baada ya kutawala kwa miaka 28 mfululizo.

Upinzani umejiongezea viti zaidi na kusonga mbele dhidi ya chama tawala cha ZANU- PF kwa mujibu wa matokeo rasmi ya uchaguzi wa bunge uliofanyika Jumamosi iliyopita nchini humo.

Tume ya uchaguzi ya Zimbabwe inasema chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change, MDC, na kundi lake lililojitenga kwa pamoja pande hizo zimeshinda viti 90 vya ubunge ikilinganishwa na viti 85 vilivyoshindwa na chama cha ZANU-PF. Matokeo ya mwisho rasmi ya uchaguzi wa bunge yanatarajiwa kutangazwa leo.

Simbabwe, Morgan Tsvangirai, Oppositionsführer
Kiongozi wa chama cha MDC Morgan TsvangiraiPicha: AP

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Harare, kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai, amekataa kudai ushindi akisema anataka kusubiri matokeo rasmi ya mwisho.

Kufikia sasa matokeo rasmi ya uchaguzi wa rais bado hayatangazwa, lakini kwa mujibu wa matokeo yasiyo rasmi Tsvangirai amemshinda rais Robert Mugabe katika uchaguzi wa rais, bunge na wa serikali za mitaa, lakini hakupata wingi wa kura kukwepa awamu ya pili ya uchaguzi.

Viongozi wa nchi mbalimbali duniani wameitolea mwito Zimbabwe iharakishe kutangaza matokeo ya mwisho rasmi ya uchaguzi huku Umoja wa Ulaya ukiwa na matumaini kuwa utawala wa miaka 28 wa rais Robert Mugabe huenda unakaribia kufika mwisho.

Marekani na Uingereza zimeongoza miito ya kuitaka serikali ya mjini Harare iheshimu uamuzi wa wananchi na kutangaza matokeo.

Großbritannien London Terror Autobombe entdeckt Gordon Brown
Waziri mkuu wa Uingereza Gordon BrownPicha: AP

Waziri mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, amesema haki ya kidemokrasia ya Wazimbabwe sharti iheshimiwe na kutaka matokeo yatolewe.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ametoa mwito kuwepo na uwazi katika zoezi la kuhesabu kura ili wazimbabwe wawe na imani na matokeo.

Wakati huo huo, askofu mkuu wa zamani wa Afrika Kusini, Desmond Tutu, amesema anaunga mkono makubaliano yatakayozuia kutokea kwa machafuko ya umwagaji damu nchini Zimbabwe kutokana na matokeo ya uchaguzi.