1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upungufu wa mafuta Gaza umeathiri mtambo wa nishati

20 Januari 2008
https://p.dw.com/p/Cv6A

GAZA: Mtambo mmoja wa kinu kikuu cha umeme katika Ukanda wa Gaza umefungwa kwa sababu ya upungufu wa mafuta.Upungufu huo umesababishwa na hatua ya Israel kufunga vivuko vyote vya mpakani.Mtambo wa pili pia huenda ukasita kufanya kazi ifikapo leo usiku.

Naibu mkurugenzi wa kinu hicho cha nishati,Rafik Maliha amesema,mtambo huo wa nishati unahudumia sehemu kubwa ya mji wa Gaza ikiwa ni pamoja na hospitali,mitambo ya maji ya kunywa na inayosafisha maji machafu na sio kwa ajili ya umeme tu.Akaongezea kuwa ni maisha ya watu wa kawaida yanayoteketezwa.

Israel inasema,imefunga vivuko vya mpakani kujibu mashambulizi ya makombora yanayorushwa kutoka Gaza kuelekea Israel.Eneo la Gaza linadhibitiwa na kundi la Hamas.Umoja wa Mataifa ukilaani hatua ya Israel kufunga vituo vya mpakani umesema,hiyo ni adhabu kwa wakaazi wote wa Gaza.