1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ureno yaingia uchaguzini

3 Juni 2011

Jumapili (05.06.2011) wapiga kura nchini Ureno wanachagua wabunge wapya katika uchaguzi wa mapema baada ya kuanguka kwa serikali hapo Mei kutokana na uamuzi wake wa kuingia kwenye mpango wa kufunga mkaja.

https://p.dw.com/p/11TeO
Waziri Mkuu wa Ureno, Jose Socrates
Waziri Mkuu wa Ureno, Jose SocratesPicha: AP

Wachunguzi wengi wamekuwa wakiziangalia wiki za hivi karibuni kwa shaka. Kwa upande mmoja, Ureno inajikuta kwenye mgogoro mkubwa kabisa wa kiuchumi.

Bila msaada wa kifedha kutoka nje, ni wazi kuwa nchi hii haiwezi tena kujimudu: uchumi utaporomoka kabisa na Wareno watajikuta hawana pesa ya kuendeshea maisha yao. Lakini kwa upande mwengine, siasa za uchaguzi zinauchukulia ukweli huu kwa namna nyengine.

Wagombea kutoka vyama vya siasa vinashindana kwenye kuangalia chanzo na suluhisho la hali hii ngumu ya kiuchumi. Kila mmoja akijiona kuwa ana suluhisho bora zaidi za chanzo anachoamini kuwa ni sababu ya kuporomoka uchumi wa Ureno.

Chama cha Kisoshaliti cha Waziri Mkuu Jose Socrates, kimetawala kwa miaka sita sasa. Kilikuwa na wingi wa asilimia 38 katika chaguzi zilizopita, licha ya hali ngumu ya kiuchumi na asilimia 16 ya ukosefu wa ajira.

Kiongozi wa Upinzani wa Ureno, Pedro Passos Coelho
Kiongozi wa Upinzani wa Ureno, Pedro Passos CoelhoPicha: AP

Socrates amekuwa akitumia mbinu za kuwatishia Wareno juu ya hatari ya serikali kushikiliwa na wapizani wake kuliko kile hasa ambacho chama chake kitafanya.

Kwenye hotuba zake amekuwa akionya kwamba kama upinzani utashinda, basi Wareno watarajie kubinafsishwa kwa kila njia kuu ya uchumi na upunguzwaji wa mfuko wa ustawi wa jamii.

"Wanachokitaka wapinzani ni kuwa na mifumo miwili ya elimu: mmoja wa masikini na mwengine wa matajiri. Kama vile ilivyokuwa wakati wa mapinduzi ya Nelken ya mwaka 1974". Amesema Socrates.

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha kiliberali, PSD, Pedro Passos Coelho, anasema kwamba ni lazima dola ijiondowe kwenye usimamizi wa mambo kadhaa, ikiwa kweli Ureno inataka kuendelea. Chama hiki kilitawala Ureno katika miaka ya '90, kikitumia sera za soko huria.

Kama PSD kitashinda, kuna makampuni kadhaa makubwa ambayo yatabinafsishwa, yakiwemo mabenki, maji, televisheni na hata reli. Lengo la chama hiki ni kuwa na serikali ndogo yenye majukumu machache sana kwenye uendeshaji wa uchumi.

"Ili serikali iweze kuwa na akiba nzuri ya fedha na kutekeleza mambo mengi, basi lazima yenyewe iwe ni kigezo. Lazima ifanye kazi nyingi zaidi na kubwa zaidi kwa kuwa na watu wachache, mifumo michache, washauri wachache, wasaidizi wachache na wapambe wachache." Anasema Coelho.

Kiongozi wa CDS-PP, Paulo Portas (katikati)
Kiongozi wa CDS-PP, Paulo Portas (katikati)Picha: picture alliance/dpa

Ikiwa mtu aatachukulia matokeo ya kura za maoni ya hivi karibuni, basi waziri mkuu ajaye wa Ureno ni Pedro Passos Coelho, maana chama chake cha PSD kina asilimia 37 ya kura hizo hadi sasa. Chama hicho pia kimeungana na chama cha kihafidhina cha CDS-PP ambacho kina asilimia 13 kikiwa katika nafasi ya tatu.

Tayari kiongozi wa CDS-PP, Paulo Portas, amesema kwamba angelipendelea kufanya kazi na PSD kuunda serikali ya mseto inayofuata siasa za mrengo wa Kati na Kushoto.

Lakini juu ya yote, serikali yoyote itakayoingia madarakani itajikuta na kazi ngumu ya kufanya, kwa sababu kuna Makubaliano ya Troika ya Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Benki Kuu ya Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa.

Wote hawa wanataka kuona serikali ya Ureno ikifanya mageuzi makubwa katika mfumo wake wa kifedha ili kuunusuru uchumi.

Hadi mwishoni mwa mwaka huu, serikali hiyo itapaswa kueleza na kuonesha namna ilivyopambana na nakisi ya matumizi, vyenginevyo itazama kwenye madeni na hivyo kufilisika.

Vyama vyote vitatu vikubwa vya Ureno, PS, PSD na CDS-PP, vinafungwa na kufanya maamuzi magumu ya kisiasa linapokuja suala hili. Na wapiga kura wao, huenda hawaujui uzito uliopo, ingawa wanataka maisha bora.

Mwandishi: Johannes Beck/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman