1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ureno yajiongezea taji la Ulaya

Sekione Kitojo
10 Juni 2019

Cristiano  Ronaldo anyakua taji  lake  la  pili  la  Ulaya , katika mashindano  ya  kwanza  ya  ligi  ya  Mataifa barani Ulaya,

https://p.dw.com/p/3K8r5
UEFA Nations League Finale - Portugal vs Niederlande
Picha: Reuters/C. Recine

 Ureno imeongeza  taji  jipya  la ligi  ya  mataifa  lililoanzishwa hivi karibuni   katika  taji  lake  la  ubingwa  wa  Euro  mwaka  2016 kwa ushindi  wa  bao 1-0 dhidi ya  Uholanzi  mjini  Porto jana  Jumapili.

UEFA Nations League Finale - Portugal vs Niederlande
Cristiano Ronaldo nahodha wa Ureno Picha: Reuters/C. Recine

Ulinzi pacha  wa  Virgil van Dijk na  Matthijs de Ligt kwa  kiasi kikubwa  ulimtia  mfukoni Cristiano Ronaldo , lakini  mshambuliaji  wa pembeni  wa  Valencia  Gonzalo Guedes aliamua  mchezo  huo wakati  shuti  lake  lilikuwa  na  nguvu  kubwa  na  kumshinda  mlinda mlango  wa  Uhloanzi Jasper Cillessen.

Ureno  ilisherehekea  kushinda  ubingwa  huo wa  ligi  ya  mataifa  ya bara  la  Ulaya kwa  kuliwasilisha  kombe  hilo katika  jengo  la halmashauri  ya  jiji  la Porto  jioni  ya  jana  Jumapili.

UEFA Nations League Finale - Portugal vs Niederlande
Bao lililoizamisha Uholanzi dhidi ya Ureno katika fainali ya kombe la ligi ya mataifa ya Ulaya Picha: Reuters/C. Recine

Maelfu  ya  mashabiki wa  kandanda  walimiminika  katika  eneo  hilo na  Cristiano  ronaldo aliwashukuru  mashabiki  hao mjini  Porto  na Ureno  kwa  jumla.

"Kwa niaba  ya  timu ya  taifa  na  wachezaji  wenzangu  wote, kwa niaba ya  rais na  makocha tungependa  kuwapa  nyie  mashabiki asante  sana kwasababu bila  nyie  isingewezekana kwa  uungaji mkono  mliotupatia katika  mchezo  wa  kwanza  dhidi  ya  Uswisi na pia  leo."

Portugal: Nations League - Niederlande vs. England
Uholanzi walishindwa kupata bao katika mchezo wa fainali dhidi ya UrenoPicha: Getty Images/D. Mouhtaropoulos

Nae  kocha  wa  Ureno  Fernando Santos  aliwashukuru  pia mashabiki  na  wanachi  wa  Ureno  kwa  kuwapa nguvu  kwa kuwaunga  mkono. Na  pia  aliwashukuru  wachezaji  wake kwa furaha  waliowapa mashabiki.

England imewasili  katika  nusu  fainali za mashindano  makubwa mawili  lakini kocha  Gareth Southgate amesema  kushindwa  kufikia fainali ya  kombe  la dunia  na  ligi  ya  mataifa  imekiacha  kikosi chake  kikiwa  hakijaridhika. Ushindi  wa  mikwaju ya  penalti  dhidi ya  Uswisi  jana  Jumapili  ulishuhudia  England  ikimaliza  katika nafasi  ya  tatu  katika  mashindano  hayo  ya  mwanzo ya  ligi  ya mataifa, nafasi  moja  bora  kuliko  kombe  la  dunia  mwaka 2018 wakati  waliposhindwa  na  Ubelgiji katika mchezo wa  kuwania medali  ya  shaba.

Portugal: Nations League - Niederlande vs. England
Katika mchezo kati ya Uholanzi dhidi ya England, washindi walikuwa Uholanzi Picha: Reuters/R. Marchante

Wakati  huo  huo  kocha  wa  Uholanzi  Ronald Koeman amesherehekea  msimu  mzuri  na  Uholanzi  licha  ya  kipigo ilichokipata  jana  Jumapili  katika  fainali  ya  ligi  ya  mataifa ya UEFA.

Koeman  amesema  kipigo  cha  bao 1-0  dhidi  ya  wenyeji Ureno katika  uwanja  wa  Estadio do Dragao hautaondoa  kitu chochote katika  kikosi  chake kutokana  na  mafnikio yaliyopata  timu  yake katika kujijenga  upya msimu  huu.