1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi, China zapinga azimio dhidi ya Syria

9 Juni 2011

China imeungana na Urusi kusema kwamba itapinga azimio linaloungwa mkono na Marekani dhidi ya Syria katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Nishati ya Atomiki unaofanyika mjini Vienna, Austria.

https://p.dw.com/p/11Xf4
Mwanajeshi wa Kituruki akiwalinda wakimbizi wa Syria
Mwanajeshi wa Kituruki akiwalinda wakimbizi wa SyriaPicha: AP

Katika taarifa yao kwa wajumbe wa bodi ya Shirika la Nishati ya Atomiki la Kimataifa hivi leo, Urusi na China zimesema kwamba hakuna haja ya kuwa na azimio dhidi ya Syria kwa sasa.

"Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina jukumu la kusimamia amani na usalama wa kimataifa na eneo la Dair Alzour halipo tena na kwa hivyo sio tena tishio kwa usalama na amani ya kimataifa. Kwa hivyo sisi hatuwezi kuunga mkono azimio hilo na hiyo ndiyo sababu kama litapigiwa kura, basi tutalipigia kura ya veto." Imesema taarifa ya Urusi.

Nayo China imetoa hoja hiyo hiyo ikisema kwamba haioni haja ya kulipeleka suala la Syria katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, China haikusema kwamba italipigia azimio hilo kura ya veto au la.

Ingawa maelezo ya azimio hili yanahusu shutuma kwamba Syria ilikuwa ikijaribu kujenga kinu cha nyuklia katika eneo liitwalo Dair Alzour, lakini, kwa undani wake, mataifa ya magharibi yanataka hatua kali dhidi ya serikali Bashar Al-Assad, ambayo kwa siku za karibuni imeripotiwa kukandamiza waandamanaji wanaodai mabadiliko nchini mwake.

Wakimbizi wa Syria nchini Uturuki
Wakimbizi wa Syria nchini UturukiPicha: picture-alliance/dpa

Mashirika ya haki za binaadamu yanasema kwa uchache vikosi vya Syria vimeshauwa watu 1,100 hadi sasa kuanzia mwezi Machi mwaka huu, huku maelfu ya wengine wakijeruhiwa na wengine wakiikimbia nchi hiyo kukimbilia Lebanon na Uturuki.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Ahmed Davutoglu, amesema kwamba nchi yake imejtayarisha kuwapokea wakimbizi hao ingawa ameitaka serikali ya Syria kuleta mageuzi yanayodaiwa na watu wake.

"Tangu mgogoro wa Syria ulipoanza, sisi tulijiandaa kwa uwezekano wa wimbi la wakimbizi. Jambo hili tumelifanyia kazi vyema. Lakini pia Syria inahitaji kutumia njia za amani kufikia demokrasia. Mabadiliko kwenye nchi ni jambo lililo wazi." Amesema Davotuglu.

Katika matukio ya karibuni zaidi, kituo cha televisheni cha Al-Jazeera kimeonesha picha za mwili wa mvulana wa miaka 15, Thamer al-Sahri, ambaye anasemekana kuteswa na kuuawa kikatili na vikosi vya Syria, baada ya kutekwa nyara mwezi Aprili.

Mwili wa mvulana huyo ulikuwa na matundu ya risasi, haukuwa na meno, jicho moja limenyofolewa, na kwa mujibu wa Al-Jazeera ulirudishwa jana kwa familia yake, huku shingo na mguu wake vikiwa vimevunjwa.

Mamia ya wakimbizi wa Syria wakiingia Uturuki
Mamia ya wakimbizi wa Syria wakiingia UturukiPicha: Picture-Alliance/dpa

Ufaransa na Uingereza zimeandaa azimio ambalo linamtaka Al-Assad kuwacha mara moja ukatili dhidi ya wapinzani na kuondoa uzio wa kijeshi katika mji kadhaa yenye maandamano. Azimio hilo pia linataka kuwekwa vikwazo vya silaha dhidi ya serikali ya Syria.

Hapo jana, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, alizionya China juu ya kulipigia kura ya veto azimio hili, akisema kwamba zitabeba lawama kwa kufanya hivyo.

Lakini, baada ya kujiepusha na kupigia kura azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lililofungua njia kwa operesheni ya kijeshi inayoendelea sasa nchini Libya, sasa Urusi inasema kwamba haitakaa tena kimya.

Urusi imekuwa ikisema imesalitiwa na wenzao wa Magharibi ambao wameligeuza azimio la kuwalinda raia wa Libya kuwa operesheni ya kuuangusha utawala wa Kanali Muammar Gaddafi, kinyume na idhini la azimio hilo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman