1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi kitovu kipya cha corona duniani

6 Mei 2020

Huku zaidi ya watu 257,000 wakiwa wamekufa kutokana na ugonjwa wa COVID-19 duniani na wengine zaidi ya milioni 3.6 wakiwa wameambukizwa, Urusi imetangaza zaidi ya maambukizi mapya 10,000 kwa siku ya nne mfululizo. 

https://p.dw.com/p/3br8U
Russland Moskau | Coronavirus | Test
Picha: Getty Images/AFP/V. Maximov

Idadi hiyo ya Urusi imeishinda ile ya Ujerumani na hivyo kuwa nchi ya sita yenye idadi kubwa ya wagonjwa waliothibitishwa duniani. Maafisa wa afya wa Urusi wamesema visa vipya vimeongezeka hadi 10,559 katika kipindi cha saa 24, na kuifanya idadi jumla kufikia 165,929. Pia kumekuwa na vifo 86 katika kipindi hicho na idadi jumla ya vifo kuwa 1,537.

Maambukizi yamekuwa yakiongezeka tangu Jumapili iliyopita, tofauti na nchi za Ulaya Magharibi ambazo taratibu zimeanza kupunguza hatua za kuzuia kuenea kwa virusi vya corona, baada ya maambukizi mapya na vifo kupungua.

Kipindi cha kusitisha shughuli za umma nchini Urusi ili kuzuia maambukizi yasisambae kinamalizika Mei 11 nchini humo na maafisa wamesema hatua hiyo inaweza ikaondolewa au ikaongezewa kulingana na takwimu za maambukizi kwenye mikoa mbalimbali.

Wanafunzi wameanza kurejea shule

Wakati hayo yakijiri, wanafunzi katika jimbo la Wuhan, China wameanza leo kwenda shule, huku wakiwa wamevalia barakoa na wakipita mmoja mmoja kwenye mashine maalum ya kupima joto.

China Coronavirus Schulen öffnen in Wuhan
Wanafunzi wakiwa shule huko Wuhan, ChinaPicha: Reuters/China Daily

Wanafunzi wa sekondari katika shule 121 ndiyo wameanza kurejea shuleni kwenye mji huo ambako virusi vya corona vilianzia. Tarehe ya kurejea wanafunzi wa shule za msingi bado haijatangazwa, ingawa baadhi ya maeneo wameanza kuwaruhusu.

Maafisa wa Wuhan wamesema wanafunzi na wafanyakazi wote wa shule lazima wawe wamepimwa virusi vya corona kabla ya kurejea shuleni na maeneo ya shule yamesafishwa na kumwagiwa dawa.

Ama kwa upande mwingine Rais wa Marekani, Donald Trump amesema nchi hiyo ina mpango wa kupunguza mamlaka ya kikosi kazi chake cha kupambana na virusi vya corona na kuelekeza nguvu zake zaidi katika kuufungua tena uchumi wake.

Pande zinazohasimiana zinastahili kutii wito wa Umoja wa Mataifa

"Nchi yetu sasa iko katika hatua nyingine ya mapambano: iliyo salama kabisa na tunaifungua tena hatua kwa hatua. Ni kuifungua tena nchi yetu. Lakini tulifanya kilicho sahihi na sasa tunaifungua tena nchi yetu na litakuwa jambo jingine muhimu sana," alisema Trump.

Teilnehmer, die an der von Indonesien geleiteten offenen Debatte über Friedenssicherungseinsätze in New York
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kikaoniPicha: Ministerium Luar Negeri

Wakati huo huo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limezitaka pande zinazohasimiana nchini Afghanistan kutii wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kusitisha mapigano mara moja ili waweze kukabiliana na janga la COVID-19 na kuhakikisha msaada wa kibinaadamu unawafika walengwa nchini humo.

Taarifa ya baraza hilo la Umoja wa Mataifa imetolewa kwenye vyombo vya habari baada ya mkutano wa faragha uliopewa taarifa kuhusu hali ya Afghanistan na naibu mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa, Ingrid Hayden.