1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi kutambua matokeo ya uchaguzi Ukraine

Abdu Said Mtullya23 Mei 2014

►Rais Putin amesema nchi yake itayatambua matokeo ya uchaguzi utakaofanyika Ukraine Jumapili. Akihutubia kwenye kongamano la kimataifa Putin pia amesema anayo matumaini mgogoro wa Ukraine utatatuliwa

https://p.dw.com/p/1C5Ru
Rais Vladimir Putin wa Urusi
Rais Vladimir Putin wa UrusiPicha: Reuters

Rais Putin aliwaambia wajumbe kwenye kongamano la masuala ya kiuchumi linalofanyika katika mji wa Urusi wa St.Petersberg kwamba Urusi inaliheshimu chaguo la watu wa Ukraine. Hata hivyo amesema kimsingi Rais wa hapo awali Viktor Yanukovich alieondolewa madarakani ndiye bado mwenye mamlaka.

Ameshauri kwamba ingelikuwa bora kuitisha kura ya maoni madhali kulingana na katiba ya sasa Yanukovich bado ndiye mwenye mamlaka. Putin amesema anatambua kwamba watu wa Ukarine wanataka kuondokana na mgogoro unaowakabili na ndiyo sababu amesema Urusi italiheshimu chaguo lao.

Matumaini juu ya suluhisho

Amesema anayo matumaini kwamba mgogoro wa Ukraine utatatuliwa na amezitaka nchi za magharibi zitumie busara kwa kushirikiana na Urusi.

Rais Putin ameeleza kwamba utafika wakati ambapo hali itakuwa ya kawaida nchini Ukraine na hivyo kuziwezesha Urusi na Marekani kuusawazisha uhusiano baina yao. Lakini pia amezilaumu nchi za magharibi kwa kusababisha Ukraine itumbukie katika alichokiita vita vya wenyewe kwa wenyewe.Juu ya vikwazo vya nchi za magharibi Rais Putin amekiri kwamba vinaiathiri biashara ya ndani ya Urusi kwa sababu mitaji kwa ajili ya kampuni imepungua.

Uchaguzi wa Rais

Rais wa kipindi cha mpito nchini Ukraine amewataka watu wote wa nchi yake wenye haki ya kupiga kura washiriki katika kupiga kura hapo Jumapili. Rais huyo wa mpito Oleksander Turchynov ambae hatagombea katika uchaguzi huo amesisitiza umuhimu wa uchaguzi wa Jumapili ambapo watu wa Ukraine watamchagua kiongozi mpya wa nchi yao. Bwana Turchynov amesema asilani hawatamruhusu yeyote kuwapora uhuru wao au kuifanya Ukraine iwe sehemu ya Urusi.

Turchynov ameeelza kuwa watu wa Ukraine wanaijenga nchi mpya ya kiulaya yenye msingi unaotokana na nguvu za mamilioni ya watu wake wenye uwezo wa kuilinda nchi yao na kile wanachokiamua. Watu 21 watakigombea kiti cha Rais hapo Jumapili. Uchunguzi wa maoni unaonyesha kwamba tajiri mkubwa Petro Poroshenko anayo matumaini makubwa ya kushinda. Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ukraine hapo awali Julia Tymoshenko yupo nyuma sana katika kura za maoni.

Mwandishi: Mtullya Abdu ape/rtre

Mhariri: Mohammed Khelef