1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sheria hiyo ni kuhakikisha Urusi inakuwa salama

16 Aprili 2019

Bunge la taifa la Urusi maarufu Duma limepitisha mswada ambao utakapokuwa sheria basi taifa hilo litabuni mfumo wake pekee wa mtandao wa Intaneti ambao utalifanya taifa hilo kutotegemea Intaneti inayotumika duniani.

https://p.dw.com/p/3Grqe
Symbolbild Urheberrecht im Internet | Grundgesetz
Picha: Imago Images/photothek

Mswada huo ambao ulipitishwa kwa kura nyingi za wabunge 307 huku 68 wakipiga kura kuupinga, utawasilishwa katika bunge kuu la Urusi ili kuidhinishwa na kisha kuwasilishwa kwa rais Vladmir Putin kutia sahihi ili kuwa sheria kamili na kuanza kutekelezwa Novemba, mosi mwaka huu.

Sheria hiyo itawezesha serikali ya Urusi kubuni miundo mbinu yao binfasi ya Intanet na kuweza kusalia mtandaoni lau kutatokea dharura ya taifa lolote kujaribu kuizima huduma za Intaneti.

Mmoja wa waandishi wa mswada huo Andrei Klishas aliye pia mwanachama wa bunge kuu aliliambia shirika la habari la DW kwamba hawana shaka Marekani ina uwezo wa kiufundi wa kuizimia Urusi huduma za Intaneti wakati wowote wakipenda kwa hivyo na wao wanajiandaa kiufundi kuhakikisha wanajilinda dhidi ya mashambulizi hayo.

Russland Moskau Andrei Klischas
Mbunge Andrei KlishasPicha: Imago Images/ITAR-TASS/A. Novoderezhkin

Mkuu wa kamati ya sera na habari Leonid Levin alisema huduma salama za intaneti ni muhimu kwa warusi na serikali kwa jumla.

"Lengo la mswada huu ni kuhakikisha Intaneti inapatikana kwa Warusi iwe ni kutoka nje ya nchi ama ndani ya nchi. Kwa njia hii, huduma ya taifa za kieletroniki, huduma za benki kutumia mfumo wa Intaneti pamoja na huduma mbali mbali za biashara ambazo wananchi wamezizoea zitafanya kazi kwa usawa kabisa bila ya kufeli. mswada huu ni kuongeza upatikanaji wa intaneti ambayo inataegemewa Urusi kwa hivyo wanalifanya hilo kuhakikisha ustawi na ubora wake," alisema Leonid.

Namna mfumo huo utakavyofanya kazi.

Hadi sasa maswala ya kiufundi ya namna miundo mbinu hiyo itakuwa hayajakuwa bayana lakini taasisi kuu ya mawasiliano ya Urusi Roskomnadzor ndio itakuwa kituo kikuu cha kufuatilia na itasimamia Intaneti hiyo kutakapotokea mashambulizi.

Mashirika yote ya kutoa huduma za Intaneti yatakuwa chini ya Roskomnadzor na watawasilisha taarifa za utumizi wa wateja wake mitandaoni.

Mswada huo pia unaeleza kwamba moja ya malengo yake ni kuhakikisha taarifa za watumizi wa Intaneti wa Urusi zinasalia nchini humo ikiwa njia moja ya kuwalinda watumizi wa mitandao ila watetetzi wa haki wanasema hili linalenga kuwathibiti wapinzani wa serikali.

Russland Moskau Proteste gegen Internet-Zensur
Waandamanaji wakishinikiza Uhuru wa Intaneti mjini Moscow Machi, 10. Picha: Getty Images/AFP/A. Nemenov

Mkurugenzi Mhandisi wa shirika la Roscomsvoboda, Stanislav Shakirov alisema wazo hili lilianza mwaka 2012 baada ya kuanza kwa vuguvugu la mapinduzi katika bara Arabu na kushika kasi wakati wa mapinduzi ya Ukraine mwaka 2014 na kutoka hapo serikali ya Urusi iliingia uoga wa mawasiliano ya mtandao wa intaneti na ndio sasa inajaribu kujilinda mapema iwapo kutakoea maandanano makubwa ya umma dhid yake.

"Hii sheria ilipitishwa baada ya China kutaka kupanua huduma zake za Inataneti, ila kwa sababu sio rahisi kutekeleza sheria hiyo hapa Urusi, uwezakano uliopo ni kwamba sheria hiyo haitaweza kutekelezwa kwa muda uliopangwa, ila itatumiwa wakati wa mapinduzi, maandamno makubwa na mengine. Intaneti itazimwa mipakani na kila kitu kuchujwa. wakati mwengine kitakachoweza kutekelezwa katika sheria hii ni kuthibiti yanayoendelea mitandaoni," alisema Stanislav.

Wazo la kuongeza uthibiti wa serikali juu ya Intaneti ni moja wapo ya malengo ya muda mrefu ya kanuni za serikali hiyo. Mwaka 2017 maafisa wa serikali walisema wanataka asilimia 95 ya shughuli za Intaneti kushughulikiwa na vyanzo vya kiufundi vya nchini humo kufikia mwaka 2020.

(DW)