1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na nchi za Magharibi zazozana utumaji misaada Syria

10 Julai 2020

Urusi na mataifa ya Magharibi wanazozana juu ya suala la kuendelea kutuma misaada ya kiutu nchini Syria hasa katika maeneo yanayothibitiwa na waasi ya kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/3f6Hy
New York UN Sicherheitsrat Sondersitzung Syrien
Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: picture-alliance/AA/T. Coskun

Ujerumani na Ubelgiji Alhamisi waliitisha kura juu ya rasimu ya azimio ambalo litaruhusu kuendelea kwa miezi sita kutuma misaada kupitia vituo viwili vya mpakani kutoka Uturuki kwenda kaskazini magharibi mwa Syria.

Azimio hilo linaungwa mkono na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, mkuu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika mengi yanayotoa misaada ya kibinadamu. Matokeo ya kura hiyo yanatarajiwa kutangazwa Ijumaa mchana.

Nord-Syrien Tel Tamer | humanitäre Krise
Raia wa Syria wakikimbia mapigano kaskazini ya nchi hiyo Picha: DW/K. Zurutuza

Bila ya kusubri matokeo hayo kutolewa, jana usiku Urusi ilianza kusambaza azimio jipya la kutafuta idhini ya kuruhusiwa kusafirisha misaada kupitia eneo moja tu la mpakani kwa mwaka.

Kupitia mfululizo wa ujumbe wa Twitter, naibu balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Dmitry Polyansky alitangaza azimio hilo jipya la Urusi, na kuzisisitiza nchi Magharibi kuliunga mkono, huku akiashiria kuwa Urusi itapinga rasimu ya azimio iliyowasilishwa na Ujerumanina na Ubelgiji kupitia kura ya turufu.

Urusi ambayo ni mshirika wa karibu wa Syria, imekuwa ikisema kwamba misaada inapaswa kusambazwa kupitia njia za ndani ya Syria zenye mapigano.

Umoja wa Mataifa wasisitiza misaada ni muhimu kwa watu wasiojiweza

Lakini Umoja wa Mataifa na makundi ya kutoa misaada ya kibinadamu wamekuwa wakisema kuwa misaada kwa ajili ya watu wenye shida wapatao milioni 2.8 haiwezi kusambazwa kwa namna hiyo.

New York | UN-Sicherheitsrat zu Krieg in Syrien | François Delattre, Botschafter Frankreich & Heiko Mass
Mabalozi wa Ufaransa na Ujerumani kwenye Umoja wa MataifaPicha: Getty Images/AFP/T.A. Clary

Azimio la Ujerumani na Ubelgiji linalopigiwa kura linatafuta idhini ya kurefusha muda wa kutuma misaada kupitia maeneo mawili ya mpakani kutoka Uturuki kwenda Bab al-Salam na Bab al-Hawa kwa miezi sita.

Rasimu ya azimio la Urusi litaruhusu kupitisha misaada kwenye kituo cha mpakani cha Bab al-Hawa, kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Balozi wa Ujerumani kwa Umoja wa Mataifa, Christoph Heusgen, amesema Jumatano kwamba wakati kituo cha mpakani cha Bab al-Hawa kinatumika kutuma misaada katika mkoa wa idlib, kituo cha mpakani cha Bab al-Salam kinafikisha misaada hadi eneo la kaskazini mwa Aleppo, ambako kuna raia wa Syria wapatao 300,000 waliopoteza makazi yao kutokana na mashambulizi.

Azimio la awali lilowasilishwa na Ujerumani na Ubelgiji kuidhinisha kusambazwa misaada nchini Syria kupitia vituo viwili vya mpakani kwa mwaka mmoja lilipata uugwaji mkono kutoka kwa wajumbe 13 kati ya 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumanne, lakini lilipigwa na Urusi pamoja na China.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/AP

Mhariri: Josephat Charo