1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na Syria zaendeleza mashambulizi

Lilian Mtono
2 Machi 2018

Vikosi vya Urusi na Syria vimeendeleza mashambulizi katika eneo linalodhibitwa na waasi la Ghouta Mashariki, wakati ambapo makubaliano tata yaliyofikiwa ya kusimamisha mapigano yakionekana kushindwa kuonyesha mafanikio.

https://p.dw.com/p/2tZQ2
Syrien Ost-Ghouta Explosions-Wolken
Picha: Reuters/B. Khabieh

Vikosi vya Urusi na Syria vimeendeleza mashambulizi katika eneo linalodhibitwa na waasi la Ghouta Mashariki, wakati ambapo makubaliano tata yaliyofikiwa ya kusimamisha mapigano yakionekana kushindwa kuonyesha mafanikio baada ya misaada ya kiutu kushindikana kuingizwa kwenye eneo hilo. Kwa upande mwingine, jeshi la Urusi limesema usitishwaji mapigano wa masaa matano umeanza kutekelezwa hii leo katika eneo hilo la Ghouta Mashariki.

Zaidi ya malori 40 yaliyobeba misaada hayakuweza kuwafikia raia takriban 400,000 wanaoishi kwenye eneo hilo linalokabiliwa na mapigano, na kuibua miito mipya ya utekelezwaji wa azimio la Umoja wa Mataifa la kusitisha mapigano ili kuruhusu misaada ya kiutu. 

Makubaliano ya kusitisha mapigano kwa masaa matano kila siku yaliyotangazwa na Urusi siku ya Jumatatu yamepelekea kupungua kwa mashambulizi yaliyosababisha vifo vya mamia ya raia katika siku chache na kuibua ghadhabu kutoka jamii ya kimataifa, mwezi uliopita.

Lakini njia zilizoandaliwa na Urusi kwa ajili ya raia kuondoka zilisalia kuwa tupu kwa siku ya tatu mfululizo, huku kukiwa na hali ya kutokuaminiana baina ya pande zote.  

Mkuu wa kikosi cha misaada ya kiutu cha Umoja wa Mataifa nchini Syria, Jan Egeland amesema ana matumaini ujumbe wa kutoa misaada wataweza kuingia Ghouta Mashariki katika kile alichoeleza kuwa ni "siku chache zijazo". 

Schweiz UN Friedensgespräche für Syrien
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Staffan de Mistura, amesema wataendelea kuomba utekelezaji wa azimio la Umoja wa Mataifa.Picha: picture-alliance/Photoshot/Xu Jinquan

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de Mistura hapo jana alipozungumza na waandishi wa habari, baada ya mkutano na mashirika ya kimataifa ya misaada ya kiutu mjini Geneva, alisema hawajakata na wala hawatakata tamaa ya kuomba utekelezwaji kamili wa azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka kusitishwa mapigano kwa siku 30 nchini Syria.

Kulingana na shirika la utetezi wa haki za binaadamu nchini Syria, ndege za kijeshi za Syria zilifanya mashambulizi ya angani jana Alhamisi kabla ya kuanza kwa usitishwaji wa mapigano majira ya saa 3 za asubuhi, na kusababisha vifo vya raia 9.

Msemaji wa kikosi cha ulinzi wa raia la nchini Syria, kijulikanacho kama "White Helmets"  Siraj Mahmud alisema imekuwa vigumu kulifikia eneo hilo, ambalo amesema, limeshambuliwa na kuharibiwa kabisa na baadhi ya raia wamefunikwa na vifusi.

Marekani hapo jana ilitoa mwito kwa Urusi kumshinikiza rais wa Syria, Bashar al-Assad na serikali yake kuheshimu jaribio la kuwahamisha raia. Msemaji wa wizara ya ulinzi, Pentagon, Dana White alisema, kushindwa kwa hatua ya usitishwaji wa mapigano kunaibua swali kuhusu wajibu wa Urusi wa kusitisha mapigano na kujadiliana kuhusu suluhu ya kisiasa. 

Urusi na Syria kwa pamoja walivituhumu vikosi vinavyoipinga serikali, vinavyopambana katika eneo la Ghouta Mashariki kwa kufanya mashambulizi kwenye njia zilizoandaliwa kwa ajili ya raia kuondoka, hivyo kuwazuia raia hao na kuwatumia kama ngao ya vita.

Jeshi la Urusi lilisema kwenye taarifa yake kwamba kwa siku tatu zilizopita, watu wengi walishindwa kuondoka Ghouta Mashariki baada ya kutekwa na makundi ya wapiganaji wenye silaha na kuwazuia kuondoka kwenye eneo hilo hatari. Raia pekee wanaoaminika kuondoka baada ya usitishwaji huu ni mke na mume wenye asili ya Pakistani, ambao walibaki Ghouta katika kipindi chote cha miaka 7 ya vita, lakini waliamua kuondoka baada ya mapigano kuongezeka.

Mwandishi: Lilian Mtono/rtre/afpe.
Mhariri: Josephat Charo