1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaahidi kuondoa majeshi yake kutoka Georgia

Charo, Josephat22 Agosti 2008

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limegawanyika kuhusu maazimio mawili yanayolenga kuumaliza mgogoro baina ya Urusi na Georgia.

https://p.dw.com/p/F2sW
Kifaru cha jeshi la Urusi kikipita karibu na bango la picha ya waziri mkuu wa Urusi Vladamir Putin mjini Tskhinvali Ossetia KusiniPicha: picture-alliance/ dpa

Ingawa Urusi imeahidi kuwaondoa wanajeshi wake kutoka mji wa Gori nchini Georgia kufikia mwendo wa saa mbili leo usiku na kuviondoa vituo vyote vya ukaguzi, imesema itawabakisha wanajeshi kadhaa watakaokuwa na jukumu la kulinda amani nchini humo.

Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema katika taarifa yake kwamba vikosi vya jeshi la Urusi vinavyowasaidia wanajeshi wake wa kulinda amani vitaondoka kutoka maeneo ya Georgia na kurejea katika jimbo la Ossetia Kusini. Hata hivyo taarifa hiyo imesema baadhi ya wanajeshi watabakia katika vituo maalum vya upekuzi kulingana naidadi inayohitajika kuhakikisha usalama unaendelea kuwepo. Hatua hiyo ya Urusi imezikasirisha nchi za magharibi.

Marekani imekulaani kuondoka kwa wanajeshi wa Urusi kutoka Georgia ikisema kunafanyika kwa mwendo wa kinyonga. Matamshi hayo yametolewa na jenerali John Craddock, kiongozi wa jeshi la Marekani barani Ulaya, wakati alipokutana na waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa Tbilisi nchini Georgia. Lakini naibu mnadhimu wa jeshi la Urusi, Anatoly Nogovitsyn, amesema leo kuondoka kwa wanajeshi wa Urusi kutoka Georgia kunafanyika kama ilivyopangwa na hakuna mpango wowote wa kuchelewesha kuondoka kwao.

Rais wa Georgia Mikheil Saakashvili amesema hatokubali kuwepo kwa maeneo ya usalama nchini mwake. Urusi inasema inahitaji kuwa na kikosi chake nchini Georgia kuzuia umwagikaji zaidi wa damu na kuwalinda raia wa jimbo la Ossetia Kusini kutokana na mashambulio ya Georgia, wengi wao wakiwa na uraia wa Urusi. Serikali ya mjini Tbilisi kwa upande wake inasema Urusi inajaribu kuyateka maeneo yaliyo himaya ya Georgia.

Huku idadi ya wanajeshi wa kulinda amani wa Urusi watakaobakia nchini Georgia ikiwa haijulikani na tofauti kati ya wanajeshi hao na wanajeshi wa kawaida wa Urusi ikiwa pia ya kutatanisha, haijabainika wazi ahadi iliyotolewa na Urusi kuviondoa vikosi vyake kutoka Georgia itakuwa na maana gani.

Baraza la usalama lagawanyika

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeshindwa kuidhinisha maazimio mawili yaliyotayarishwa na Ufaransa na kusainiwa na Urusi na Georgia yanayolenga kuumaliza mzozo kati ya nchi hizo mbili. Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin, aliwasilisha azimio la Urusi alilosema linajumulisha kanuni sita zilizo katika makubaliano yaliyofikwa kati ya Urusi na Georgia ambayo yalisimamiwa na Ufaransa.

´´Katika ibara ya kwanza ya azimio hili kuna maelezo ya kanuni sita zilizokubaliwa na rais wa Urusi Dimtry Medvedev na rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy na baadaye kuungwa mkono na Georgia, Abkhazia na Ossetia Kusini. Kwa hiyo tunadhani ni azimio zuri ambalo baraza la usalama linatakiwa lilipitishe.´´

Balozi Churkin amesema baada ya kikao cha baraza la usalama la umoja huo mjini New York Marekani, kwamba ana matumaini wanachama wa baraza hilo wataliunga mkono azimio la Urusi. Azimizo hilo lililenga kupinga azimio la Ufaransa linalotaka Urusi iondoe wanajeshi wake kutoka Georgia na iheshimu mipaka yake. Wanadiplomasia wengi wa baraza la usalama hawakuliunga mkono pendekezo la Urusi lakini badala yake wakataka kutayarishwe azimio litakaloumaliza mgogoro kati ya Georgia na Urusi.