1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaigomea ICC kesi ya Greenpeace

25 Oktoba 2013

Serikali ya Urusi imesema kuwa haitafika katika kesi dhidi yao kwenye mahakama ya kimataifa ya ICC Uholanzi.

https://p.dw.com/p/1A613
Meli ya Uholanzi iliyokuwa na wanamazingira Urusi.
Meli ya Uholanzi iliyokuwa na wanamazingira Urusi.Picha: picture-alliance/AP/Greenpeace International

Serikali ya Urusi imesema kuwa haitafika katika kesi dhidi yao kwenye mahakama ya kimataifa ya ICC Uholanzi, ambapo inakabiliwa na mashitaka ya kuikamata meli ya Uholanzi, iliyokuwa na wanamazingira wa kimataifa katika eneo la bandari ya mji wa Murmansk nchini Urusi.

Wanaharakati hao wa kimazingira pamoja na waandishi wa habari, walikuwa katika ziara ya mgomo wa kupinga shughuli za uchimbaji mafuta katika eneo la bahari huru, zinazoendeshwa na kampuni ya uchimbaji mafuta ya Serikali ya Urusi.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema, nchi yake imeitaarifu Uholanzi na mahakama ya kimataifa ya ICC kuwa, kuhusiana na sheria ya mipaka ya bahari, haitashiriki katika kesi hiyo na kuongeza kuwa Urusi itashughulikia hali hii inayojitokeza baina ya nchi hizo mbili, bila ya kufafanua kwamba watahitaji nini kwa maridhiano ya baadae.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi
Waziri wa mambo ya nje wa UrusiPicha: Reuters

Taswira Mpya ya uhusiano

Uamuzi huo unapelekea hatua nyingine ya kuongezeka kwa mvutano baina ya nchi hizo mbili zenye uhusiano wa kibiashara kwa muda mrefu, ambapo kwa sasa kuna mfululizo wa visa wanavyofanyiana nchi hizo, ikiwa ni pamoja na afisa wa kibalozi wa Urusi aliyetiwa nguvuni nchini uholanzi kwa madai ya kumtesa mtoto wake na kwa upande wa Urusi, wametishia kuzuia uingizwaji bidhaa kutoka Uholanzi na wiki iliyopita afisa wa kibalozi wa uholanzi nchini Urusi alipigwa nyumbani kwake mjini Moscow na mtu asiejulikana na kumwandikia ujumbe katika kioo wa kumtaka kuunga mkono haki za mashoga.

Uholanzi ilitangaza kuishitaki serikali ya Urusi katika mahakama ya kimataifa ya ICC kufuatia kukamatwa kwa meli yake katika bandari ya Murmansk nchini Urusi mwezi uliopita , iliyokuwa na wanaharakati wa mazingira wa kimataifa kutoka nchi 18, na waandishi wa habari, waliokuwa katika harakati za kupinga mradi unaoendeshwa na Urusi wa kuchimba mafuta katika eneo huru la bahari . Kesi hiyo katika mahakama ya kimataifa ya ICC iliyofunguliwa na Uholanzi, inaitaka serikali ya Urusi kuiachia meli hiyo pamoja na wanaharakati wakiwamo waandishi wa habari waliokuwa humo. kesi hiyo inatarajiwa kuanza kusikilizwa wiki mbili au tatu kuanzia sasa.

Aidha serikali ya Urusi imewafungulia mashitaka ya uharamia wanaharakati hao, ambayo kwa sheria za Urusi makosa ya uharamia adhabu yake ni kifungo cha miaka 15 jela.

Nchi hizo mbili zenye mvutano,

Mahakama ya icc
Mahakama ya icc

tayari zimefikia hatua ya kutishiana kuvunja mahusiano ya kibiashara na kibalozi. Mapema mwezi huu afisa wa ngazi ya juu wa afya wa Urusi, alitoa onyo kuwa Moscow inaweza kuzuia uingiaji wa bidhaa za vyakula kutoka uholanzi kwa sababu za usalama wa kiafya kwa walaji.

Pia Urusi imeshutumiwa kwa kutumia uhusiano wa kibiashara kama silaha katika masuala ya kidiplomasia ,ambapo iliwahi kusimamisha uingiaji wa vyakula kutoka nchi za umoja wa Ulaya na nchi zilizokua katika Muungano wa Jamhuri ya Ki-sovieti, ambao sasa umesambaratika.

Mvutano huo kati ya Urusi na uholanzi ulipamba moto wakati polisi mjini The Hague walipomkamata afisa wa kibalozi wa Urusi nchini Uholanzi, kwa madai ya kumtesa mwanawe ambapo baadae walimwachia afisa huyo. Hata hivyo serikali ya uholanzi iliomba radhi kwa hilo kutokana na kukiuka masharti ya mkataba wa Vienna, unaohusu makubaliano ya taratibu za kidiplomasia za kimataifa

Mwandishi:Diana Kago/AFP/DPA
Mhariri: Moahammed Abdul-Rahman