1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaishutumu Marekani kwa shambulio la Syria

Admin.WagnerD12 Aprili 2017

Mwanadiplomasia mkuu wa Urusi lameituhumu Marekani kwa kufanya shambulio dhidi ya vikosi vya Rais Bashar al Assad wa Syria wakati alipokutana na mwenzake wa Marekani Rex Tillerson ambaye yuko mjini Moscow.

https://p.dw.com/p/2b8ZN
USA Russland Tillerson bei Lawrow
Picha: Reuters/M. Shemetov

 

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov ambaye hakumpa makaribisho ya shangwe waziri mwenzake wa Marekani amesema Urusi ilikuwa inajaribu kuelewa dhamira hasa za utawala wa Trump.

Amesema Urusi ina masuali mengi  kuhusu fikra zenye utata mkubwa sana na zenye kukanganya kutoka kwa serikali ya Marekani.

 Lavrov amesema "Nitakuwa mkweli kwamba tumekuwa na masuali mengi kuhusiana na fikra zenye utata mkubwa na mara nyengine zenye kukanganya katika suala zima la uhusiano baina ya nchi mbili na agenda ya kimataifa. Ni muhimu kwetu kufahamu msimamo wa Marekani juu ya dhamira za serikali yako. Tunataraji tutapita njia hiyo leo hii".

Lavrov amesema wameshuhudia hatua za kushtusha sana za kushambuliwa kwa Syria akikusudia makombora yaliyovurumishwa na Marekani kutoka kwenye meli yake yalioamuriwa na Rais Donald Trump kumuadhibu Assad kwa kutumia silaha za sumu. Amesema wanaona ni jambo muhimu kabisa kuzuwiya hatari ya kurudia kwa kitendo hicho katika kipindi cha usoni.

Mwanzo mgumu

USA Russland Tillerson bei Lawrow
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov.Picha: picture-alliance/AP Photo/I. Sekretarev

Ni mwanzo mgumu kwa ziara hiyo ya Tillerson ambayo ni ya kwanza kufanywa nchini Urusi na waziri wa serikali ya Marekani. Tillerson amekiri kwamba mataifa hayo mawili yenye nguvu duniani yanatafautiana sana jambo ambalo amesema limekwamisha ushirikiano lakini ameelezea matumaini yake kwamba mazungumzo yao yatapunguza tofauti hizo.Tillerson amesema wote wamekubaliana kwamba njia zao za mawasiliano daima zitakuwa wazi.

Tillerson amesema "Mikutano yetu leo hii inakuja katika wakati muhimu wa uhusiano kwamba tunaweza kuyakinisha maeneo ya malengo ya pamoja, maeneo ya maslahi ya pamoja hata kama mbinu tunazozitumia pengine ikawa ni tafauti. Na kuyakinisha zaidi maeneo yenye tofauti kubwa ili kwamba tufahamu vizuri zaidi kwa nini tofauti hizo zinakuwepo na kuna matarajio gani pengine ya kupunguza tofauti hizo."

Wakati huo huo Trump amekiambia kituo cha habari za kibiashara cha Fox kwamba Marekani haina mipango ya kujihusisha zaidi nchini Syria na kwamba ilifanya hivyo tu kwa sababu ya shambulio la silaha za sumu lililofanyika wiki iliyopita na kusababisha maafa. Uturuki imesema ilikuwa na vipimo vyenye kuonyesha kwamba gesi ya sarin ilitumika.

Katika mahojiano Trump amesema  "Je tutajihusisha nchini Syria, hapana" m lakini ameongeza kusema kwamba iwapo itaona wametumia gesi itabidi wachukuwe hatua.Hali ya mvutano yakini ulioigubika safari hiyo ya Tillerson inaonyesha kutanuka kwa pengo kati ya mahasimu wao wa zamani wa vita baridi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP

Mhariri:Josephat Charo