1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yasikitishwa na uamuzi wa IOC

Bruce Amani
5 Februari 2018

Urusi imesema imesikitishwa sana na uamuzi wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki wa kutowaruhusu wanamichezo wa Urusi waliofutiwa madai ya kutumia dawa za kuongeza misuli nguvu kushiriki katika Michezo ijayo ya Olimpiki.

https://p.dw.com/p/2s9gL
Olympia Russland Fan Symbolbild Ausschluß
Picha: picture-alliance/Chicago Tribune/B. Cassella

IOC imesema leo kuwa wanamichezo 15 wa Urusi na makocha ambao hatua ya kupigwa marufuku ya maisha ilibatilishwa na mahakama ya CAS hawataalikwa katika michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi itakayoanza tarehe 9 mwezi juu mjini Pyeongchang, Korea Kusini. Thomas Bach ni rais wa IOC

Heshima ya kualikwa haitokani tu na kuondolewa vikwazo, kwa hivyo hatujawaalika. Tunataka kutenda haki kwa wanamichezo wote, bila kujali paspoti zao. Wanamichezo safi wa Urusi walioalikwa wanaweza kuwa mabalozi wa kizazi kipya: wanaweza kuwa mfano mzuri. Wanaweza kudhihirisha kwa wanamichezo wenzao kuwa ukiwa msafi unazawadiwa na sio kuadhibiwa. Sasa ni jukumu la Urusi kuonyesha kweli inataka kukaribishwa tena kwenye Michezo ya Olimpiki.

IOC imesema bado inasubiri kupewa maelezo kamili kuhusu nini kilifanya mahakama ya CAS kuchukua uamuzi huo wa Februari mosi wa kuyafuta madai ya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini dhidi ya wanamichezo wa Urusi.

IOC yaionya AIBA

IOC Olympia Russland Doping
Rais wa IOC Thomas BachPicha: Reuters/D. Balibouse

Mchezo wa ndondi huenda ukapigwa TKO yaani technical knockout katika Michezo ijayo ya Olimpiki kama Kamati ya Kimatzaifa ya Olimpiki – IOC haitaridhika kuwa matatizo yanayoukumba mchezo huo kuhusiana na masuala ya kifedha na usimamizi yametatuliwa. Akizungumza mjini Pyeongyang, Korea Kusini kabla ya Michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi itakayoanza wiki ijayo, Rais wa IOC Thomas Bach ameonya kuwa kamati yake ina wasiwasi mkubwa kuhusu namna mchezo wa masumbwi unavyoongozwa na akasema kuwa shirika lake liko tayari kufanya maamuzi mazito

Bodi kuu ya IOC inathibitisha kuanzishwa kwa uchunguzi unaofanywa na Afisa mkuu wa maadili wa IOC kuhusiana na usimamizi wa AIBA. IOC inasitisha utoaji wa malipo yoyote ya kifedha kwa AIBA ikiwa ni pamoja na malipo ya moja kwa moja yanayohusiana na mshikamano wa Olimpiki.  IOC imesitisha mawasiliano yote na AIBA isipokuwa yale yanayohusu utendaji kazi ambayo ni muhimu katika utekelezaji wa maamuzi ya IOC. IOC inahitaji kupokea ripoti nyingine kutoka kwa AIBA ifikapo Aprili 30, 2018

Chama cha kimataifa cha mchezo wa ndondi – AIBA hakinaweza kutoa tamko mpaka sasa kuhusu onyo hilo la Bach. AIBA imekumbwa na malumbano ya ndani, wakati aliyekuwa makamu wa rais CK Wu kwanza aliachishwa kazi kwa muda na kisha akajiuzulu Novemba mwaka jana baada ya mgogoro mkali na kamati yake kuu. AIBA imetangaza siku ya Jumamosi Gafur Rahimov kuwa kaimu rais wake, kufuatia kujiuzulu kwa ghafla kwa kaimu rais Franco Falcinelli.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Gakuba, Daniel