1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaushambulia mji wa Odesa

Grace Kabogo
16 Mei 2022

Jeshi la Ukraine limesema kuwa shambulizi la anga la Urusi limeushambulia mji wa bandari wa Odesa na kuharibu makaazi ya kitalii, ambapo watu watatu wamejeruhiwa.

https://p.dw.com/p/4BNKs
Nächtliche Luftangriffe an Odesa
Picha: Oleksandr Gimanov/AFP

Kwa mujibu wa jeshi la Ukraine, shambulizi hilo la leo lilililenga daraja la Mto Dniester ambalo lilishambuliwa pia kwa mashambulizi ya awali. Mji wa Odesa uliopo katika Bahari Nyeusi, ambao hapo awali ulikuwa kivutio maarufu cha watalii kutoka Urusi, umekuwa ukikoswakoswa na mashambulizi yanayoendelea katika eneo la kaskazini na mashariki mwa Ukraine. Hata hivyo, mashambulizi ya awali ya Urusi yamesababisha uharibifu na vifo katika mji huo.

Huku hayo yakijiri, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amemteua Meja Jenerali Ihor Tantsyura kuwa mkuu wa vikosi vya jeshi la ulinzi vinavyolisaidia jeshi la Ukraine kupambana na uvamizi wa Urusi, kuchukua nafasi ya Yurir Halushkin.

Taarifa iliyotolewa na wizara ya ulinzi, haijaelezea sababu zozote za uteuzi huo. Wizara hiyo imemuelezea Tantsyura kama afisa mwenye ujuzi na uzoefu wa kutosha ambaye awali alikuwa mkuu wa vikosi vya nchi kavu vya Ukraine.

Ukriane-Krieg Charkiw | Soldat nach Rückeroberung
Mwanajeshi wa Ukraine akifanya doria KharkivPicha: Mstyslav Chernov/AP/picture alliance

Aidha, wizara hiyo imesema katika tarifa tofauti kwamba vikosi vya jeshi la ulinzi vya Ukraine vimesonga mbele kuelekea kwenye mpaka na Urusi, baada ya kuvirudisha nyuma vikosi vya Urusi vinavyoushambulia mji wa kaskazini mashariki wa Kharkiv.

Kamanda wa jeshi la Ukraine katika mkoa wa Luhansk amesema mashambulizi ya usiku wa kuamkia leo yaliilenga hospitali moja ya Severodonetsk na kuwaua watu wawili na kuwajeruhi wengine tisa, akiwemo mtoto. Amesema mashambulizi hayo ya usiku pia yaliilenga miji mingine.

Sweden kuomba kujiunga NATO

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Sweden Magdalena Andersson amesema leo kuwa nchi yake itawasilisha ombi la kujiunga na Jumuia ya Kujihami ya NATO.

"Baada ya mjadala bungeni, tumeamua kufanya mkutano wa ziada wa serikali, ambapo tumefanya maamuzi mawili. Kwanza, serikali imeamua kuijulisha NATO kwamba Sweden inataka kuwa mwanachama wa muungano huo wa kijeshi. Na hivi karibuni, balozi wa Sweden NATO ataijulisha jumuia hiyo kuhusu hili. Baada ya hapo, mazungumzo ya kujiunga yataanza," alifafanua Andersson.

Hiyo ni hatua ya mabadiliko ya kihistoria ya miongo kadhaa kwa nchi hiyo kutofungamana na upande wowote ule kijeshi.

Schweden Premierministerin Magdalena Andersson
Waziri Mkuu wa Sweden Magdalena AnderssonPicha: Michele Tantussi/REUTERS

Naye Rais wa Urusi, Vladmir Putin amesema hana tatizo na Sweden na Finland kutaka kujiunga na NATO, lakini atachukua hatua katika kukabiliana na utanuzi wowote wa miundombinu ya kijeshi ya NATO kwenye nchi hizo.

Ama kwa upande mwingine Umoja wa Ulaya na Marekani leo zimekubaliana kuratibu zaidi matendo yao ili kupunguza athari za vita vya Urusi nchini Ukraine kwenye uchumi wa dunia.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa leo baada ya kikao cha Baraza la Biashara na Teknolojia la Umoja wa Ulaya na Marekani imeeleza kuwa wamejitolea kufanya kazi pamoja na Ukraine kuujenga upya uchumi wake na kuwezesha biashara na uwekezaji.

Pia wanadiplomasia wakuu wa Umoja wa Ulaya wamesema hakuna uhakika kwamba umoja huo utakubaliana haraka awamu mpya ya vikwazo dhidi ya Urusi, huku kundi dogo la nchi zinazoongozwa na Hungary, zikipinga vikwazo vya mafuta.

(AFP, AP, Reuters, DW)