1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yazidisha mashambulio dhidi ya Georgia

Saumu Mwasimba11 Agosti 2008

Wakaazi wa Gori waukimbia mji huo

https://p.dw.com/p/Eu5c
Vifaru vya kijeshi vya Urusi vikielekea katika mji wa Tskhinvali, Ossetia kusini.Picha: picture-alliance/ dpa

Urusi inaendelea na mashambulizi yake dhidi ya Georgia licha ya Georgia kuamua kusitisha mashambulio katika jimbo lake lililojitenga la Ossetia Kusini na kuitisha mazungumzo ya amani na Urusi.

Taarifa zinasema Wanajeshi wa Urussi wameingia kwenye mji wa Gori wa Georgia na wameanza mashambulio.Wakaazi wa mji huo wamekimbia mashambulio ya kijeshi ya Urussi.Rais Gorge W Bush wa Marekani amemwambia waziri mkuu wa Urussi Vladmir Putin kwamba mashambulio hayo hayakubaliki.

Aidha mapema hii leo ndege za kivita za Urusi zilishambulia kambi ya kikosi maalum cha Georgia karibu mji mkuu wa nchi hiyo Tbilisi.Taarifa zinasema Urusi pia imezamisha boti ya makombora ya Georgia ikidai kwamba boti hiyo ilijaribu kushambulia meli zake katika bahari ya Black Sea.

Rais wa Georgia Mikheil Saakashvili amesema vifaru vya Urusi vimevuka mpaka wa jimbo la Ossetia na kuingia katika ardhi yake.Wanajeshi wa Urusi pia wanaripotiwa kuudhibiti kikamilifu mji mkuu wa Ossetia Kusini wa Tskhinvali. Wakati huohuo baraza la usalama la Umoja wa mataifa limekuwa na kikao cha dharura juu ya mzozo huu ambapo Marekani imeionya Urusi kwamba huenda ikaumia ikiwa itakataa kuchangia katika kutafuta suluhisho la amani kwenye mzozo huo.

Kwa upande mwingine Umoja wa Ulaya umesema hautokubali kuangalia vita vikiendelea karibu na eneo lake kwahivyo uko tayari kusaidia kutafuta suluhisho la kidiplomasia katika mzozo huo.Wakati huohuo Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy anatazamiwa kwenda Moscow wiki hii kama sehemu ya juhudi za kuumaliza mzozo huu.Ufaransa ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya.