1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yazidisha mashambulizi katika mji wa Odessa

3 Mei 2022

Urusi imefanya mashambulizi mapya katika bandari muhimu ya Odessa wakati ambapo Marekani imetahadharisha kuwa Urusi inajiandaa kuzingira rasmi maeneo yanayopiganiwa kwa sasa mashariki mwa Ukraine.

https://p.dw.com/p/4AkOL
Ukraine Luftangriffe in Odessa
Picha: Bulent Kilic/AFP/Getty Images

Baada ya kushindwa kuuteka mji wa Kyiv Urusi imeupeleka uvamizi wake ambao umedumu kwa zaidi ya miezi miwili sasa katika maeneo ya Ukraine ambayo Kirusi ndicho kinachozungumzwa na kuongeza shinikizo huko Odessa, mji wa kitamaduni ulio na bandari muhimu katika Bahari Nyeusi.

Manispaa ya mji wa Odessa kupitia mtandao wa Telegram imesema shambulizi la Urusi limepiga nyumba moja iliyokuwa makaazi ya watu watano, mvulana mmoja mwenye miaka 15 ameuwawa kutokana na shambulizi hilo na msichana amelazwa hospitali kutokana na majeraha aliyoyapata.

Makabiliano makali zaidi yatarajiwa Lugansk

Gavana wa eneo la mashariki la Lugansk amesema anatarajia makabiliano makali zaidi kuelekea maadhimisho ya Mei 9, siku ambayo Urusi inasherehekea ushindi ilioupata mwaka 1945 dhidi ya Wanazi wa Ujerumani.

Ila Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema majeshi ya Urusi hayatofanya mabadiliko katika uvamizi wake siku yoyote ile ikiwemo siku hiyo ya Mei 9 ambayo inaitwa Siku ya Ushindi huko Urusi.

Lawrow sieht "reale Gefahr" eines dritten Weltkrieges
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei LavrovPicha: Attila Kisbenedek/AFP/Getty Images

Lakini Marekani inaonya kwamba Urusi inajiandaa kuzingira miji ya Lugansk na Donetsk.

Haya yanafanyika wakati ambapo Umoja wa Ulaya unasema unajiandaa kwa kukatwa kabisa kwa usambazaji wa gesi ya Urusi wakati ambapo umoja huo unaandaa vikwazo vingine dhidi ya Urusi ambavyo bila shaka vitamghadhabisha Rais Vladimir Putin.

Umoja wa Ulaya umechukua uamuzi huu baada ya mazungumzo na nchi wanachama hapo Jumatatu ambapo uliwataarifu wajiandae kwa kukatwa kabisa kwa usambazaji wa gesi kutoka Urusi kwa kuwa hawawezi kukubali matakwa ya Urusi kwamba bidhaa hiyo ilipwe kwa sarafu ya Urusi ya ruble.

Vilabu vya kandanda Urusi kutoshiriki mashindano ya UEFA

Katika pigo jengine kwa Urusi, Shirikisho la Kandanda Barani Ulaya UEFA limetangaza kwamba vilabu vya Urusi vimepigwa marufuku kushiriki katika mashindano ya UEFA ikiwemo Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya, Champions League, msimu ujao.

Shinikizo laongezeka kwa Ujerumani kutuma silaha nzito Ukraine

Hayo yakiarifiwa waziri wa mambo ya nje wa Israel Yair Lapid amelaani matamshi ya waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov alipodai kwamba Adolf Hitler alikuwa na "damu ya Kiyahudi." Israel imemuita balozi wa Urusi nchini humo kulizungumzia suala hilo.

Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwaacha zaidi ya watu milioni 13 bila makao katika vita ambavyo havijawahi kushuhudiwa barani Ulaya kwa vizazi kadhaa. Miongoni mwa miji iliyoharibiwa pakubwa na Mariupol ambapo wengi wameaga dunia na waliosalia hawapati chakula, maji na madawa kwa urahisi.

Chanzo: AFPE/APE