1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usalama waimarishwa siku ya Ashura

4 Novemba 2014

Maelfu ya waumini wa madhehebu ya Shia nchini Iraq wamekusanyika kwenye mji mtakatifu wa Karbala kwa ajili ya kushiriki Ashura kukumbuka mauaji ya Imam Hussein,mjukuu wa mtume Mohammad

https://p.dw.com/p/1DgTm
Waislamu washia wakiadhimisha Ashura kwenye msikiti wa Imam Hussein mjini Karbala
Waislamu washia wakiadhimisha Ashura kwenye msikiti wa Imam Hussein mjini KarbalaPicha: AFP/Getty Images/M. Sawaf

Kumbukumbu ya siku ya Ashura inahusiana na mauaji ya mjukuu wa mtume Mohammad yaliyofanywa na jeshi la Kalifa Yazid mwaka wa 680 baada ya Nabii Issa (AD),na hivyo hukumbukwa hadi hii leo na waislamu wa madhehebu ya shia kwa kufanyika ibada maalum. Shughuli hiyo nchini Iraq imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi yanayofanywa na wasunni wenye itikadi kali katika miaka iliyopita ingawa mwaka huu kumbukumbu hizo zinafanyika katika wakati ambapo kundi la wapiganaji wenye itikadi kali wakisunni wanaojiita dola la kiislamu IS wakishikilia sehemu kubwa ya nchi hiyo.

Mamia kwa maelfu ya maafisa wa usalama pamoja na wanamgambo wanaoshirikiana nao wamepelekwa kwenye maeneo mbali mbali kuwalinda waumini katika kile ambacho kinaonekana kama ni mtihani mkubwa kwa serikali mpya ya waziri mkuu Haidar al Abadi. Akizungumza na shirika la habari la ufaransa AFP gavana wa mji mtakatifu kwa washia wa Karbala Aqil-al-Turaihi amesema mamia kwa maelfu ya mahujaji kutoka mikoa yote ya Iraq pamoja na wengine kutoka nchi za kiarabu na za kigeni wamekusanyika mjini Karbala kushiriki kumbukumbu hizo za kifo cha Imam Hussein.

Waziri mkuu wa Iraq Haider al Abadi akiwa pamoja na kiongozi mkuu wa Iran Khayatollah Ali Khamenei
Waziri mkuu wa Iraq Haider al Abadi akiwa pamoja na kiongozi mkuu wa Iran Khayatollah Ali KhameneiPicha: picture-alliance/dpa

Mamia ya waumini wakiume wamevalia shuka nyeupe wameshiriki ibada inayofahamika kama Tatbeer ambapo wanajikatakata vichwa vyao kwa kutumia upanga na mishale kama ishara ya kuomboleza kuuwawa kwa Imam Hussein mjukuu wa Mtume Mohammad. Hata hivyo ni mahujaji wachache wanaofanya kitendo hicho ambacho huwaacha nguo zao zikiwa zimelowa damu.Ikumbukwe kwamba hatua hiyo inakosolewa na kulaaniwa na baadhi ya viongozi wa kidini wa madhehebu hayo ya shia. Kwa upande mwingine maelfu ya mahujaji wanakusanyika kusikiliza hadithi za imam Hussein pamoja na vita alivyoshiriki ambako aliuwawa na kutokana na hilo waumini hujiadhibu kwa kujipiga vichwa vyao na kulia kama ishara ya kuomboleza na kujutia kifo hicho cha Imam Hussein.

Makundi ya wasuni wenye itikadi kali ambao wamekuwa wakiwaangalia washia kama wapinzani wa dini wamekuwa wakiwauwa mahujaji kadhaa katika maadhimisho ya siku hii ya Ashura. Hata hivyo hatari kubwa imejitokeza mwaka huu wakati wanamgambo wa kundi la dola la kiislamu walipoyateka maeneo kadhaa ya Iraq kaskazini na magharibi mwa Baghad hadi kusini mwa mji huo karibu kabisa na njia ya kuelekea kwenye eneo kunakofanyika kumbukumbu hizo. Ama kundi hilo la dola la Kiislamu limetajwa na mashirika ya Kimataifa ya kutetea haki za binadamu kuhusika katika kuwatesa watoto wakikurdi waliowateka nyara mapema mwaka huu kaskazini mwa mji wa Kobani huko Syria.

Mapambano dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu,Iraq
Mapambano dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu,IraqPicha: Reuters

Shirika la Human Rights Watch limetoa ripoti yake hiyo iliyoandikwa kufuatia mahojiano walioyafanya na watoto wengi waliokuwa ni miongoni mwa vijana 150 wakikurdi kutoka Kobani. Halikadhalika taarifa zinasema kundi hilo limewaachia huru wakurdi 93 kutoka Syria katika mji wa Kobani waliotekwa nyara mnamo mwezi Februari.Walioachiwa huru ni miongoni mwa wakurdi 160 waliotekwa nyara wakisafiri kutoka Syria kuelekea Kurdistan nchini Iraq.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman