1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usawa katika Siasa ni Demokrasia Halali

P.Martin19 Aprili 2008

Ripoti mpya iliyotolewa na Umoja wa Mabunge Duniani-(IPU) wenye makao yake mjini Geneva,Uswisi imeonyesha kuwa wanawake wanabadili vipaumbele bungeni kila pembe ya dunia.

https://p.dw.com/p/Dki6

Ripoti hiyo pia imedhihirisha kuwa utaratibu wa kuingiza wanawake zaidi bungeni unakwenda pole pole mno.Ikiitwa "Usawa katika Siasa" ripoti hiyo ilitolewa kwenye mkutano mkuu wa IPU uliofanywa Cape Town,Afrika Kusini kuanzia April 13 hadi 18.IPU ni shirika linalojumuisha mabunge kote duniani.

Mkutano wa kwanza wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa kuhusu wanawake,ulipofanywa mwaka 1975 nchini Mexico idadi ya wabunge wa kike duniani ilikuwa kama asilimia 11. Na hadi mwaka huu wa 2008 hakuna maendeleo makubwa yaliyofanywa,kwani ripoti ya IPU inaonyesha kuwa wanawake walio bungeni ni takriban asilimia 18 tu.Hiyo ni idadi ndogo mno kulinganishwa na asilimia 30 inayodhaniwa na wengi kuwa ndio inayohitajiwa ili wanawake waweze kuwa na usemi bungeni.

Hata hivyo,maendeleo hayo madogo yasigubike hatua zilizopigwa katika baadhi ya nchi,hasa barani Afrika na Asia.Katika kanda hizo mbili wanawake sasa wanadhibiti asilimia 17 ya viti bungeni.Rwanda ndio imepiga fora kote duniani.Nchini humo asilimia 49 ya wabunge ni wanawake.Katika mataifa yaliyofanikiwa kuwa na wabunge wa kike kwa zaidi ya asilimia 30,nusu ni nchi zinazoendelea.Katibu Mkuu wa IPU Anders Johnsson amesema,nchi zinazoendelea na zinazoinukia zimefanya maendeleo makubwa,wakati mataifa yanayoitwa "wazee wa demokrasia" hayakusonga mbele hivyo.

Ripoti ya IPU imeonyesha kuwa miongoni mwa wanawake wanaostahili kugombea ubunge,ni wachache tu walio tayari kufanya hivyo.Uchunguzi wa jumla uliofanywa umeonyesha kuwa miongoni mwa wanaume,sababu kuu ya kutoingia katika siasa ni kutoamini kuwavutia wapiga kura. Lakini upande wa wanawake,sababu ni majukumu ya nyumbani.Walipouliziwa hatua gani zitasaidia kuwavutia wanawake zaidi katika siasa walisema,hasa ni fikra kuhusu nafasi ya wanawake katika jamii inayohitaji kubadilishwa kwa njia ya elimu.Vile vile kuwepo mahala maalum pa kuwahudumia watoto ili wanawake wawe huru kufuatiliza majukumu yao ya kisiasa.

Kizingiti kingine kwa wanawake ni kwamba vyama vingi vya kisasa havina mwongozo maalum kuhusu uteuzi wa wagombea uchaguzi.Pasipo kuwepo mwongozo dhahiri basi maamuzi hupitishwa na wakuu wa vyama ambao mara nyingi ni wanaume na ni kama klabu yao.Hapo ndio kwenye kishindo kwani si rahisi kwa wanawake kujipenyeza ndani ya klabu hiyo.Kwa maoni ya Katibu Mkuu wa IPU Anders Johnsson si jamii na mfumo wa bunge tu unaohitaji kurekebishwa.Hata vyama vya kisiasa vinapaswa kufanya mageuzi ili wanawake zaidi waweze kushiriki katika jukwaa la kisiasa.Ripoti hiyo kuhusu usawa katika siasa inasema,wanaume na wanawake wanapaswa kukubali na kukiri kwamba kwa kuwajumuisha wanawake kwa usawa katika taratibu za bunge,haitonufaisha jamii tu bali ni lazima kwa demokrasia iliyo halali.