1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ushindi wa Macron waviparaganyisha vyama vikubwa Ufaransa

Iddi Ssessanga
12 Juni 2017

Chama cha Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kiko njiani kupata wingi mkubwa viti vya bunge, baada ya duru ya kwanza ya uchaguzi Jumapili kuviacha katika mparaganyiko vyama vikongwe.

https://p.dw.com/p/2eVRn
Frankreich Macrons neue Partei La Republique en Marche
Picha: Getty Images/AFP/G. van der Hasselt

Matokeo rasmi ya uchaguzi nchini Ufaransa yamethibitisha kuwa chama cha mrengo wa wastani cha rais Emmanuel Macron kinaongoza katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa bunge la taifa. Chama hicho cha Jamhuri Yasonga Mbele -LREM na washirika wake wa mrengo wa kati wameshinda asilimia 32.32 ya kura kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na wizara ya mambo ya ndani.

Chama cha siasa za wastani za mrengo wa kulia cha Republican kiko katika nafasi ya pili kwa asilimia 21.56, kikifuatiwa na kile cha siasa kali za kizalendo za mrengo wa kulia cha National Front kinachoongozwa na Marine Le Pen kilichopata asilimia 13.2, huku chama cha mrengo mkali wa kushoto cha "Ufaransa Thabiti" chake Jean Luc Melenchon kikiwa na asilimia 11 ya kura. chama cha Kisashalisti na vyama vingine vya mrengo wa kushoto vinashika mkia kwa kugawana asilimia 9.5 kati yao.

Frankreich | Parlamentswahlen - Präsident Emmanuel Macron beim Verlassen des Wahllokals
Rais Emmanuel Macron akisalimiana na wapigakura baada ya kupiga kura yake siku ya Jumapili.Picha: picture-alliance/abaca/E. Blondet

'Ujumbe wa wapigakura uko wazi'

Akitangaza ushindi wa chama cha LREM katika duru hiyo ya kwanza ya uchaguzi ambao unatazamiwa kupangua na kupanga upya siasa za Ufaransa, waziri mkuu Eduard Philippe alisema licha ya ushiriki mdogo wa asilimia 49 tu ya wapigakura, ujumbe wa watu wa Ufaransa ulikuwa wazi - kwamba wanaunga mkono mradi wa rais wa mwanzo mpya, umoja na ufufuaji, na hivyo wanahitaji bunge lenye sura mpya.

"Kwa muda wa mwezi mmoja rais wa Jamhuri ameonyesha mfano mzuri wa kujiamini, nia na ujasiri nchini Ufaransa na pia kwenye ngazi ya kimataifa. Serikali kwa upande wake inaonyesha, kupitia wajumbe wake, muundo mpya kabisaa, na imedhamiria kuitumikia Ufaransa na kushughulikia matarajio ya Wafaransa," alisema waziri mkuu Philippe.

Hofu ya kukosekana upinzani wa kweli

Wachunguzi wa maoni ya wapigakura wamekadiria kwamba kambi ya Macron inaweza kupata hadi viti 450 kati ya jumla ya viti 577, na kwamba upinzani ndani ya bunge huenda ukawa mdogo na uliogawanyika. Uchaguzi huu umefanyika zaidi ya mwezi mmoja baada ya Macron mwenye umri wa miaka 39 kuchaguliwa kuwa rais mdogo zaidi wa Ufaransa, alipomshinda Marine Le Pen kwa asilimia 66 dhidi ya 34 katika duru ya pili ya uchaguzi.

Chama cha Kisoshalisti kilichoshikilia madaraka katika bunge lililopita na washirika wake wamepigwa na mshangao, ambapo makadirio yanaonyesha wingi wao wa viti 314 unaweza kupungua na kubakiza hadi viti 20 na yumkini siyo zaidi ya 30 katika bunge jipya. Kiongozi wa chama cha Kisoshalisti Jean-Christophe Cambadelis ameonya kuwa chama cha Macron kinaweza kuishia kuongoza bila upinzani wowote wa maana.

Parlamentswahl in Frankreich 2017 Reaktion von Francois Baroin
Kiongozi wa chama cha Republican Francois Baroin akizungumza baada ya kutangazwa kwa matokeo ya duru ya kwanza ya uchaguzi wa Bunge ambapo chama chake pia kimekubwa na sunami ya Macron.Picha: Imago

Mrengo wa kulia nako ni vilio tu

Kwa upande wa kulia, wahafidhina wa chama cha Republican walikuwa pia wanaugulia maumivu, wakitabiriwa kupata viti visivyozidi 110, na pengine vikawa vichache hadi 70, badala ya viti 215 walivyokuwa navyo katika bunge linalomaliza muda wake.

Chama cha Le Pen cha National Front hakionekani kubadili nguvu yake katika uchaguzi wa rais kuwa chochote zaidi ya idadi ndogo tu ya viti bungeni, na bila shaka idadi isiyotosha kukifanya kuwa chama cha upinzani chenye nguvu.

Hayo ndiyo yalikuwa matumaini ya Le Pen baada ya kuingia kwa mara ya kwanza katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais dhidi ya Macron mwezi Mei. Le Pen alilalamika kwamba mfumo wa uchaguzi hauwakilishi kikamilifu matakwa ya wapigakura, kwa sababu chama chake kilishinda asilimia 14 ya kura lakini hakikuweza kuongeza kwenye idadi ya wabunge wawili kiliokuwa nao katika bunge lililopita.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae

Mhariri: Daniel Gakuba