1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usitishaji mapigano mashakani Gaza

1 Agosti 2014

Usitishaji wa mapigano wa saa 72 kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza uko mashakani masaa machache baada ya kuanza kutekelezwa wakati Hamas ikisema shambulio la kifaru cha Israel limeuwa watu 25.

https://p.dw.com/p/1CnMb
Mwanamke wa Kipalestina akilia baada ya kuona nyumba yake imeangamizwa na mashambulizi ya Israel katika mji wa Beit Hanoun kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.
Mwanamke wa Kipalestina akilia baada ya kuona nyumba yake imeangamizwa na mashambulizi ya Israel katika mji wa Beit Hanoun kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.Picha: Reuters

Usitishaji huo wa mapigano uliotangazwa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na Umoja wa Mataifa umeanza saa mbili asubuhi baada ya mapigano makali kuuwa Wapalestina 17 na wanajeshi watano wa Israel. Israel na Hamas zimekubaliana kusitisha operesheni zote kuu na kuchukuwa hatua za kujihami tu.

Akiutolea ufafanuzi mpango huo waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema Wapelstina walioko Gaza wataweza kupatiwa chakula,madawa na msaada wa kibinaadamu, kuwahudumia ndugu zao waliojeruhiwa na kuzika wale waliouwawa.

Hata hivyo waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani ametahadharisha kwamba hakuna uhakikisho kwamba usitishaji huo wa mapigano utakomesha vita hivyo ambavyo hivi sasa vimeingia wiki ya nne.

Muda mfupi kabla ya saa nne asubuhi vifaru vya Israel vilishambulia eneo la mashariki la mji wa Rafah ulioko kusini ya Gaza na kuuwa watu 25 na kujeruhi wengine 15.Msemaji wa jeshi la Israel amesema bila ya kutowa ufafanuzi kwamba kulikuwa na mashambuliano makali ya risasi katika eneo la Rafah.

Kulikuwa na takriban usitishaji wa mpigano mara nne chini ya misingi ya utu kulikotangazwa tokea kuanza kwa mzozo huo lakini makubaliano ya kusitisha mapigano yote yalivunjwa muda mchache kutokana na kuanza upya kwa mapigano.Usitishaji huu wa mapigano wa leo wa saa 72 ni muda mrefu kuwahi kutangazwa.

Hamas kuzuwiya operesheni za Israel

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Hamas Gazi Hamad amesema hawatokubali kuiachia Israel kuendelea kufanya operesheni zake huko Gaza.Amesema "Huko ni kwenda kinyume na makubaliano hayo na Israel haina haki kuendelea na opresheni hizo za kijeshi kwa sababu watazitumia kubomowa nyumba zaidi na kuifanya ifanye itakavyo na wakati huo huo Wapalestina wakitakiwa wanyamaze kimya hii si haki.Iwapo Israel itaendelea na operesheni hizo ni haki yetu kujihami na kuchukuwa hatua zinazohitajika."

Wapalestina wakikimbia mshambulizi ya Israel huko Rafah ,Gaza Kusini.(31.07.2014)
Wapalestina wakikimbia mshambulizi ya Israel huko Rafah ,Gaza Kusini.(31.07.2014)Picha: picture-alliance/AP

Chini ya makubaliano hayo ya kusitisha mapigano vikosi vya Israel vilioko Gaza vinaweza kuendelea kuyaharibu mahandaki yanayopakana na mpaka wao wenye ulinzi mkali lakini yale tu yalioko safu ya ulinzi ya Israel na yanayoelekea ndani ya ardhi ya Israel.

Waziri Mkuu wa Israel Banjamin Netanyahu hapo jana ameapa kuungamaiza mtandao wa mahandaki wa Hamas aidha kwa kuwepo ustishaji wa mapigano au hata bila ya usitishaji wa mapigano.

Vita vya Gaza vimeuwa zaidi ya Wapalestina 1,450 wengi wao wakiwa raia na zaidi ya Waisrael 60 wengi wao wakiwa ni wanajeshi.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef