1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usitishaji mapigano mashariki mwa Ukraine mashakani

7 Septemba 2014

Miripuko mikubwa katika mji muhimu mashariki mwa Ukraine jana Jumamosi(06.09.2014) imezusha hofu kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya serikali na wapiganaji wanaotaka kujitenga tayari yamevunjika.

https://p.dw.com/p/1D8Gx
Ostukraine: Brüchige Waffenruhe bei Mariupol
Mripuko mkubwa mashariki mwa UkrainePicha: Getty Images

Miripuko kadhaa ilisikika na moshi mkubwa ulionekana katika mji wa Mariupol , mji wa bandari unaoshikiliwa na majeshi ya serikali mashariki mwa nchi hiyo. Kituo cha upekuzi barabarani kinachoshikiliwa na waungaji mkono serikali ya Ukraine kilionekana kuchomwa moto jioni ya Jumamosi, kwa mujibu wa mwandishi habari wa shirika la habari la AFP aliyeko katika eneo hilo.

Mapigano hayo yaliyoanza tena yanakuja saa chache baada ya mazungumzo ya simu kati ya rais wa Ukraine Petro Poroshenko na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin , ambao wamekubaliana kwamba makubaliano yaliyotiwa saini siku ya Ijumaa "kwa kiasi kikubwa yanaendelea".

Waffenstillstand in der Ostukraine
Usitishaji mapigano unaendeleaPicha: picture-alliance/dpa/R.Pilipey

Makubaliano hayo yenye vipengee 12 ni ya kwanza kupata kuungwa mkono na serikali ya Ukraine na Moscow baada ya miezi mitano ya mapigano ambapo watu 2,800 wameuwawa na kuzusha mzozo mkubwa katika uhusiano wa mataifa ya magharibi na mashariki kwa kipindi kirefu.

Hofu ya kuvunjika makubaliano

Lakini mapambano hayo mapya yanatishia kurejea hali ya usitishaji mapigano ulioamuliwa na serikali mjini Kiev Juni ,na kuvunjika katika muda wa siku chache tu.

Pande zote mbili zimelaumiana jana Jumamosi kwa kuvunja makubaliano hayo masaa kadhaa baada ya kutiwa saini katika mji mkuu wa Belarus , Minsk. Wapiganaji wanaotaka kujitenga wanaounga mkono Urusi wanasisitiza hawata kubali kuacha matakwa yao ya kuwa na taifa huru katika eneo la viwanda la mashariki mwa Ukraine likiwa na mahusiano ya kidiplomasia na kibiashara na Urusi.

"Tunataka rais wetu, sarafu yetu na mfumo wetu wa kibenki," mpiganaji anayeunga mkono Urusi anayejulikana kama Oleg ameliambia shirika la habari la AFP katika mji ulioko Donetsk wa Yasynuvata.

Waffenstillstand in der Ostukraine
Wapiganaji wakiangalia hali ilivyo ya usitishaji mapiganoPicha: Reuters/M.Shemetov

"Hii ndio njia pekee. Hakuna njia nyingine." Viongozi wa mataifa ya magharibi yanaishutumu Urusi kwa kuchochea uasi kwa kupeleka idadi kubwa ya wanajeshi na zana za kivita ndani ya Ukraine --- madai ambayo Urusi imekuwa mara zote ikiyakana.

Licha ya usitishaji mapigano , Marekani na Umoja wa Ulaya zimekubaliana kuimarisha vikwazo dhidi ya Urusi , na NATO imeidhinisha jeshi litakalochukua hatua kwa haraka kwa lengo la kuyahakikishia mataifa ya Ulaya mashariki ambayo yana wasi wasi na hatua za Urusi.

Urusi yauonya Umoja wa Ulaya

Urusi imeonya itajibu iwapo Umoja wa Ulaya utaweka vikwazo zaidi, na kuushutumu Umoja huo kwa kuunga mkono "ghafla ya vita" mjini Kiev.

Petro Poroshenko
Rais Petro Poroshenko wa UkrainePicha: picture-alliance/dpa/M.Palinchak

"Badala ya kutafuta kwa gharama zote njia za kuuathiri uchumi wa mataifa yao na Urusi, Umoja wa Ulaya utakuwa unafanya vizuri kuunga mkono ufufuaji wa uchumi wa jimbo la Donbass" la mashariki mwa Ukraine, wizara ya mambo ya kigeni imesema siku ya Jumamosi.

Maelezo kamili ya makubaliano ya amani hayakutolewa , licha ya baadhi ya masharti kutaka pande zote mbili kuanza kuondoa majeshi yao kutoka katika maeneo ya vita na kubadilishana wafungwa kuazia jana Jumamosi.

Urusi pia inaruhusiwa kupeleka msaada wa kibinadamu katika miji iliyoharibiwa mashariki mwa Ukraine , hatua ambayo ilikuwa inapingwa na Ukraine kwa hofu kuwa milolongo ya malori inaweza kutumiwa kuingiza silaha.

Hakuna ishara iwapo vipengee vyote vimetekelezwa hadi sasa siku ya Jumamosi. Wakati huo huo NATO imeendelea na luteka ya kijeshi mashariki mwa Ulaya jana Jumamosi yenye lengo la kupeleka ujumbe wa "wazi na wenye nguvu" kwa Urusi kwamba jumuiya hiyo ya kujihami itazilinda nchi wanachama wake.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Bruce Amani