1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utawala wa Assad ukingoni - NATO

14 Desemba 2012

Jumuiya ya Kujihami ya NATO imesema Rais Bashar al Assad huenda akashindwa kuendelea kubakia madarakani hivi karibuni, huku Marekani ikipeleka makombora ya Patrioit mpakani mwa Uturuki na Syria.

https://p.dw.com/p/172Gw
Katibu mkuu wa NATO Anders Rasmussen
Katibu mkuu wa NATO Anders RasmussenPicha: Reuters

Kauli hiyo ya NATO imekuja wakati zikitolewa taarifa kwamba Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Leon Pannett, akiwa ameshatia saini amri ya kupelekwa makombora ya Partiot pamoja na wanajeshi 400 nchini Uturuki kulinda ardhi ya nchi hiyo dhidi ya mashambulizi ya roketi kutoka Syria.

Kwa mujibu wa gazeti la The New York Times, makombora sita ya Patriot yamepangwa kupelekwa nchini Uturuki chini ya usimamizi wa kikosi cha NATO yakitokea Marekani, Ujerumani na Uholanzi kufikia mwishoni mwa mwezi wa Januari.

Mapambano ya miezi 20 dhidi ya Rais Assad yamekuwa chanzo kikubwa cha umwagikaji wa damu nchini humo huku mapigano makali yakizuka mara kwa mara katika eneo la kaskazini la Syria linalopakana na Uturuki, nchi inayowaunga mkono waasi.

Makombora ya Patriot
Makombora ya PatriotPicha: AP

Mfumo wa makombora hayo ya Patriot, kwa hivyo, umedhamiriwa kupelekwa kuzuia ndege za kijeshi au makombora ya jeshi la serikali ya Syria katika eneo hilo.

Uturuki ilituma ombi ramsi kwa NATO kupeleka makombora hayo katika eneo lake la mpakani na Syria ambako inahofiwa hali ya usalama huenda ikazidi kuzorota wakati wanajeshi wa Syria wakiongeza nguvu zao kuwadhibiti waasi ambao wamekuwa wakijificha katika eneo hilo la Uturuki.

Huku utekelezwaji wa hatua hiyo ukisubiriwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Kijeshi la Jumuiya ya NATO, Jenerali Knud Bartels, ametoa kauli inayoashiria kwamba utawala wa Assad unaelekea ukingoni. Jenetali Bartels amesem Rais Assad huenda asiweze kubakia tena madarakani lakini akasita kueleza ni lini Rais huyo anafikiriwa kuondoka madarakani.

Rais wa Syria Bashar al-Assad
Rais wa Syria Bashar al-AssadPicha: AFP/Getty Images

Lakini kauli hiyo inaonekana kutofautiana na mtazamo uliotolewa na Urusi leo Ijumaa. Tangazo la wizara ya mambo ya nje imesema haijabadili msimamo wake juu ya mzozo huo, taarifa ambayo imeonekana kujitenga kwa wizara hiyo na matamshi ya Naibu Waziri Mikhail Bogdanov hapo jana aliyesema Assad ataondoka madarakani na kwamba waasi wanaonekana kuelekea kushinda vita vya Syria.

Hata hivyo wizara hiyo ya mambo ya nje ya Urussi imesema naibu waziri Bogdanov hakutoa taarifa hiyo.Aidha wizara hiyo imesisitiza kwamba serikali ya nchi hiyo inataka kuona yanafikiwa makubaliano chini ya misingi ya mwafaka uliofikiwa katika mkutano wa kimataifa mapema mwaka huu.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/Reuters/AFP
Mhariri: Josephat Charo