1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utawala wa Gaddafi wakaribia kufikia kikomo

22 Agosti 2011

Mapigano makali yanaripotiwa kuendelea katika mji mkuu Tripoli, huku utawala wa Gaddafi ukiapa kuulinda mji huo dhidi ya waasi.

https://p.dw.com/p/12L6Y
Kiongozi wa Libya, Muammar GaddafiPicha: dapd

Waasi nchini Libya wameingia katikati ya mji mkuu Tripoli huku utawala wa miaka 42 wa kiongozi wa nchi hiyo, kanali Muammar Gaddafi ukikaribia kuanguka. Katibu mkuu wa jumuiya ya kujihami ya NATO, Anders Fogh Rasmussen, amesema jumuiya hiyo iko tayari kushirikiana na baraza la kitaifa la mpito linaloongozwa na waasi.

Wakati huo huo, mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita, ICC, mjini The Hague, Uholanzi, imethibitisha kukamatwa kwa mtoto wa kiume wa Gaddafi, Seif al Islam. Mtoto mwingine wa kiongozi huyo, Mohammed, amezingirwa na waasi nyumbani mwake Tripoli pamoja na familia yake. Gaddafi mwenyewe hajulikani aliko, lakini amekataa kukubali kushindwa na badala yake amewataka Walibya wauokoe mji mkuu Tripoli.

Bürgerkrieg in Libyen Erfolg der Rebellen ARCHIV
Mwana wa Gaddafi, Seif al-Islam GadhafiPicha: dapd

Rais wa Marekani Barack Obama amesema utawala wa Gaddafi umefikia ukingoni na kumtaka aondoke madarakani ili kuepusha damu zaidi kumwagika. Amewataka waasi kuheshimu haki za binadamu, kuonyesha uongozi mzuri, kuhifadhi taasisi za Libya na kuelekea katika demokrasia.