1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utawala wa visiwa vya Comoro wataka kiongozi muasi kurejeshwa nchini humo.

27 Machi 2008
https://p.dw.com/p/DVpK

Moroni.

Utawala wa visiwa vya Comoro umedai leo kuwa unataka Ufaransa imrejeshe kiongozi muasi ambaye anatakiwa katika visiwa hivyo kujibu mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu na majeshi yalifyatua mabomu ya kutoa machozi kuwazuwia waandamanaji dhidi ya kufanya ghasia katika ubalozi wa Ufaransa.

Mohammed Bakar , mwenye umri wa miaka 45 ambaye alijitangaza kuwa kiongozi wa Anzuan , alikimbilia katika kisiwa cha karibu kinachomilikiwa na Ufaransa cha Mayotte baada ya mashambulizi makali yaliyofanywa na wanajeshi wa jeshi la umoja wa Afrika na yale ya Comoro.

Serikali ya Ufaransa imesema kuwa kiongozi huyo muasi ameomba hifadhi ya kisiasa.

Ufaransa , pamoja na Marekani , ziliunga mkono operesheni hiyo kumuondoa madarakani kiongozi huyo muasi, ambaye ni mwanajeshi wa zamani aliyepata mafunzo Ufaransa na ambaye alitwaa madaraka mwaka 2001 na kung'ang'ania hadi alipofanya uchaguzi ambao ulielezwa kuwa ni batili mwaka jana katika kisiwa cha Anzouan, moja kati ya visiwa vitatu vinavyounda Comoro.

Wengi wa wakaazi wa Anzouan wanamshutumu kwa kutawala kwa kutumia vitisho na ghasia na kuendea kinyume haki za binadamu kwa kutumia vitendo vya mateso.