1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utoaji mimba usio salama.

Halima Nyanza14 Oktoba 2009

Uchunguzi uliofanywa duniani unaonesha kuwa wanawake wapatao elfu 70, hufariki dunia kwa mwaka, kutokana na utoaji mimba usio salama, huku wanawake wengine milioni tano wakipata matibabu kutokana na matatizo hayo.

https://p.dw.com/p/K6EL
Wanawake wa India ambao pia nao wametajwa katika ripoti ya Taasisis ya Guttmacher, kutokana na kukabiliwa pia na utoaji mimba usio salama.Picha: AP

Ripoti hiyo iliyotolewa na Taasisi ya Guttmacher yenye makao yake nchini Marekani, ambayo inaangalia maendeleo ya afya ya uzazi na jinsia, kupitia utafiti pamoja na sera ya elimu, imebainisha kuwa idadi ya utoaji mimba duniani imeshuka kutoka milioni 45.5 katika kipindi cha mwaka 1995, hadi kufikia milioni 41.6 mwaka 2003.

Lakini hata hivyo kushuka kwa idadi hiyo, hakujapunguza idadi ya vifo.

Rais wa taasisi hiyo Sharon Camp, anasema nusu ya vifo vinavyotokana na utoaji mimba usio salama vinatokea katika bara la Afrika, na kufuatiwa na eneo la kusini mwa bara la Asia.

Anasema licha ya kwamba utoaji mimba nchini India na Bangladesh, umehalalishwa, lakini sio wanawake wote kutoka katika nchi hizo wanapata huduma iliyo bora.

Dokta Camp anasisitiza kuwa kinga ya haraka yenye kupatikana bila ya matatizo ni vidonge vya kuzuia mimba, kwa kufafanua kuwa mimba inapotolewa ina maana kuwa ujauzito huo haukutakiwa na kwamba iwapo wanawake wataweka kipaumbele kujizuia wasipate mimba, ikishindikana ndio watoe aidha kiuhalali ama kinyume na sheria, vifo vinavyotokana na utoaji mimba usio salama vitapungua.

Ripoti hiyo iliyotolewa na taasisi hiyo ya Guttmacher iliyopewa jina la ''Utoaji mimba duniani kote'', inabainisha kuwa nchi 19 zimepunguza vikwazo katika sheria za utoaji mimba tangu mwaka 1997, lakini licha ya mwelekeo huo, asilimia 40 ya wanawake duniani kote wanaishi katika nchi ambazo kuna sheria kali za utoaji mimba, na ni katika nchi zinazoendelea.

Katika bara la Afrika licha ya maendeleo yaliyopatikana katika baadhi ya nchi, asilimia 92 ya wanawake wenye kuweza kubeba ujauzito wanaishi chini ya sheria kali za utoaji mimba, ambapo Amerika ya kusini ni asilimia 97.

Dokta Sharon Camp anasisitiza kuwa nchi nyingi ambazo ziko huru na sheria hizo za utoaji mimba, ni zile zilizopo katika nchi zilizoendelea na kwamba nchi nane za Afrika ndizo zimebadilisha sheria zao, ikiwemo Afrika kusini na Ethiopia.

Anasema sheria mpya kuhusiana na utoaji mimba nchini Afrika kusini imepata matokeo yenye kuvutia, kutokana na kupungua kwa utoaji mimba usio salama na visa vya utoaji mimba kwa ujumla, licha ya kwamba bado si wanawake wa vijiji vyote wenye uwezo wa kupata huduma bora.

Ripoti hiyo inasema vitendo vya utoaji mimba kwa kutodhamiria vimepungua kutoka asilimia 69 kwa wanawake elfu moja wenye umri wa miaka 15-44, katika kipindi cha mwaka 1995, hadi kufikia asilimia 55 kwa kila wanawake 1,000 katika kipindi cha mwaka 2008, na kwamba idadi ya wanawake walioolewa wanaotumia vidonge vya kuzuia mimba imeongezeka kutoka asilimia 54 katika kipindi cha mwaka 1990, hadi kufikia asilimia 63 mwaka 2003, lakini ni asilimia 28 tu, ya wanawake walioolewa katika nchi za Afrika ndio wanaofanya hivyo.

Mwandishi: Halima Nyanza(ips)

Mhariri:Abdul-Rahman