1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Uturuki kurejesha majukumu kwa Rais

18 Agosti 2015

Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu atarejesha jukumu la kuunda serikali ijayo kwa Rais Tayyip Erdogan baada ya wiki za mazungumzo na vyama vya upinzani kushindwa kufikia suluhisho la kuunda serikali ya muungano

https://p.dw.com/p/1GH5n
Türkei Koalitionsgespräche Devlet Bahceli und Ahmet Davutoglu
Picha: Reuters/A. Altan

Mkwamo huo wa kisiasa huenda ukaamanisha kuwa Uturuki itaandaa uchaguzi wa mapema. Chini ya katiba ya nchi hiyo, Rais Erdogan huenda akalivunja baraza la mawaziri la muda aliloliunda Davutoglu na kutoa wito wa kuundwa serikali ya mpito ya kugawana madaraka ili kuiongoza Uturuki kueleka katika uchaguzi mpya ikiwa hakutakuwa na muafaka ifikapo Agosti 23.

Mpango kama huo wa muda mfupi kinadharia huenda ukavikabidhi nafasi za mawaziri vyama vinne vilivyo na migawanyiko mikubwa ya kiitikadi, na kuukwamisha mchakato wa kutunga sera hivyo kuiyumbisha zaidi nchi hiyo ambayo tayari thamani ya sarafu yake ya lira imeshuka kabisa.

Chama tawala cha AK kilipoteza wingi wake wa viti bungeni katika uchaguzi wa Juni 7, na kukiacha bila uwezo wa kuunda serikali kwa mara ya kwanza tangu kilipoingia madarakani mwaka wa 2002. Hali hiyo iliitumbukiza Uturuki katika hali ya sintofahamu ambayo haijawahi kuonekana tangu serikali tete za muungano za miaka ya 90.

Türkei Ankara Parlament Davutoglu
Bunge la Uturuki mjini AnkaraPicha: picture-alliance/dpa

Davutoglu alikutana jana na kiongozi wa chama cha upinzani cha siasa za mrengo wa kulia – Nationalist Movement – MHP Devlet Bahceli katika juhudi za mwisho kujaribu kukubaliana kuunda serikali inayoweza kufanya kazi, lakini kiongozi huyo alikataa mapendekezo yote yaliyowekwa mezani. Baada ya mkutano wao, Davutoglu alisema "Nnaamini kuwa nimewasilisha kila pendekezo lililopo kwa vyama vya upinzani. Tumejadili mapendekezo manne lakini hakuna makubaliano ya kuchukua hatua mpya. Ninaheshimu kabisa maamuzi ya viongozi wa upinzani lakini baada ya kujadili hali hii na kamati kuu ya chama cha AK; nitakutana na rais na nitamrejeshea jukumu ikiwezekana baada ya kushauriana naye".

Mazungumzo na chama kikuu cha upinzani cha Republican People's – CHP yalivunjika wiki iliyopita, wakati chama cha nne bungeni, kinachowaunga mkono Wakurdi cha People's Democratic – HDP, kwa muda mrefu kilifuta uwezekano wowote wa kuunda serikali ya muungano na chama tawala AKP.

Erdogan huenda sasa kinadharia akakabidhi jukumu la kuunda serikali ijayo kwa CHP, chama cha pili kwa ukubwa nchini Uturuki, ijapokuwa pia kuna uwezekano mkubwa kuwa huenda asififaulu kuunda serikali ya muungano kabla ya muda wa mwisho wa Agosti 23.

Bunge pia huenda likapiga kura kuliruhusu baraza la sasa la mawaziri kuendelea kufanya kazi hadi uchaguzi mpya utakapoandaliwa, lakini chama cha MHP tayari kimesema kuwa kitapinga hatua kama hiyo na vyama vingine vya upinzani havina motisha kubwa ya kufanya tofauti na hilo.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Josephat Charo