1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki: Kuungana kwa upinzani kwamtia kishindo Erdogan

Lilian Mtono
22 Juni 2018

Rais wa Uturuki, Recep Tayipp Erdogan anasema anataka kutumia mbinu iliyotumika enzi ya Ottoman ili kuwadhoofisha wapinzani wake katika uchaguzi wa rais wa bunge unaofanyika Jumapili ijayo.

https://p.dw.com/p/304K9
Türkei Kundgebung zur Unterstützung von Erdogan in Istanbul
Picha: Reuters/O. Orsal

Kofi maarufu la uso lililotambulika enzi ya utawala wa Ottoman, ambalo lilikuwa kali na lenye kasi kama umeme, lililotumiwa na wanajeshi wakati wa Utawala wa Ottoman lililowafanya maadui zake kuanguka na kupoteza fahamu, wakiwemo wanaume na hata farasi, ni mbinu ambayo rais wa Uturuki, Recep Tayipp Erdogan ameahidi kuitumia katika uchaguzi wa urais na wabunge unaotarajiwa kufanyika jumapili ijayo, ili kuwaangusha wapinzani wake. 

Rais wa Uturuki, Recep Tayipp Erdogan aliapa kuitumia mbinu kama hiyo dhidi ya wapinzani wake katika uchaguzi wa rais na bunge utakaofanyika Jumapili ijayo. Erdogan alisikia akiuambia mkutano wa hadhara kama wapo tayari kuwapiga wapinzani kwa kofi hilo la Ottoman ifikapo Juni 24. Alisema watalifanyia kazi hilo, na hawatasimama wala kurudi nyuma. 

Lakini pia wapinzani wake pia wamejizatiti, na wakiendelea kufanya kampeni kali kote nchini humo wakiwahamasisha wapiga kura wao, ambapo kwa muda mrefu upinzani umekuwa dhaifu.

Waturuki kwa mara ya kwanza watapiga kura kwa wakati mmoja ya kumchagua rais na wabunge, katika chaguzi ambazo zinatajwa kuwa ni za muhimu zaidi katika historia ya karibuni ya taifa hilo.

Türkei Kundgebung zur Unterstützung von Erdogan in Istanbul
Waturuki wanapiga kura katika uchaguzi muhimu wakati taifa hilo likipitia magezúzi makubwa ya kisiasa.Picha: Reuters/O. Orsal

Chaguzi hizo zinafanyika wakati kuna hali ya tahadhari, ambayo ilitangazwa baada ya jaribio la mapinduzi la Julai 2016. Mgombea mmoja wa urais Selahattin Demirtas, ambaye ni kiongozi mwenza wa zamani wa chama kinachoungwa mkono na Wakurdi cha Kurdish People's Democratic Party, HDP yeye yuko kizuizini. Upinzani umepata nguvu kuliko ilivyowahi kutokea hapo nyuma, na kudhihirisha kitisho cha kweli kwa uwepo wa Erdogan. 

Chaguzi hizo pia zitaimarisha hatua ya mpito ya Uturuki kutoka kwenye mfumo wa mamlaka ya bunge hadi mfumo unaompa mamlaka makubwa rais, kufuatia kura ya maoni ya marekebisho ya katiba mnamo mwezi Aprili, 2017, ambapo Erdogan alishinda kwa tofauti ndogo. Kuuweka mfumo huo, yalikuwa ni matamanio yake ya muda mrefu na hivi sasa amefunga hatma yake ya kisiasa kwenye mfumo huo.

Türkei Muharrem Ince der Republikanische Volkspartei (CHP)
Muharrem Ince, mpinzani nambari moja wa Erdogan nchini humo.Picha: picture alliance/AP Photo/CHP/Z. Koseoglu

Muharrem Ince wa chama cha Republican People's Party, CPH, aliyeibuka mbele ya umma kumpinga kiongozi huyo ndio mpinzani na kitisho kikubwa zaidi kwa Erdogan. Amewaambia wafuasi wake kwenye mkutano wa hadhara kuwa kiongozi huyo amechoka na hafai tena.

Mpinzani aliyeko kizuizini, Demirtas ameliambia shirika la habari la dpa hivi karibuni kwenye mahojiano ya kimaandishi aliyofanya kupitia wanasheria wake kwamba malengo yake ni kuilinda demokrasia dhidi ya utawala wa mtu mmoja, na kuahidi kuhakikisha anafanikiwa kuurejesha mfumo wa utawala wa bunge.  

Hapo awali chaguzi zilipangwa kufanyika Novemba 2019. Lakini kamari aliyoicheza Erdogan ya kuitisha uchaguzi wa mapema huenda ikawa inatokana na hofu kwamba uchumi unaweza kuzorota zaidi. Thamani ya sarafu ya Uturuki ya lira imeshuka mwaka huu, na pia kukishuhudiwa mfumuko wa bei.

Mwanzilishi mwenza wa taasisi inayojihusisha na masuala ya sera za kigeni ya Foreign Policy Interrupted, Elmira Bayrasli amesema Erdogan aliitisha uchaguzi wa mapema kwa sababu hakutaka kuwapa jukwaa wapinzani ili kuwasilisha ujumbe wao kwa umma. Lakini alipiga vibaya mahesabu yake alisema. Hivi sasa upinzani umeungana pamoja kukabiliana na chama tawala cha Justice and Development, AKP, aliongeza Bayrasli.

Kura ya maoni ya hivi karibuni hata hivyo inaonyesha kuwa Erdogan atashinda kwenye uchaguzi huo kwa wingi wa kura, miongoni mwa wagombea 6 wa urais. Kile ambacho bado si dhahiri, ni iwapo atashinda kwenye duru ya kwanza, na iwapo kutakuwa na duru ya pili Julai 8, ama nini kitatokea kwa chama cha AKP katika uchaguzi wa wabunge. 

Mwandishi: Lilian Mtono/DPAE

Mhariri: Iddi Ssessanga